Hakika Sisi tumeanza kuiteremsha Qur'ani katika usiku ulio jaa kheri, wenye baraka nyingi, kwani ni mwendo wetu kuonya kwa kuwatuma Mitume na kuteremsha Vitabu.
Katika usiku huu wenye baraka hupambanuliwa baina ya mambo yote yenye hikima, na Qur'ani ndio kilele cha hikima, na ndio pambanuo baina ya kweli na uwongo. Na kwa hivyo ndio ikateremshwa katika usiku huo.
Nakusudia kwa jambo hili, yaani jambo kuu lenye kutoka kwetu kama ilivyo kwisha pita hukumu ya mpango wetu. Kwani ni shani yetu kutuma Mitume kwa Vitabu ili kuwafikishia waja wetu.
Kwa ajili ya rehema ya Mola wako Mlezi kwa waja wake, amewatuma Mitume kwa watu wawafikishie uwongofu wake, kwani hakika Yeye peke yake, ndiye Mwenye kusikia kila cha kusikiwa, Mwenye kujua kila cha kujuulikana.
Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi na vilio baina yao, ikiwa nyinyi mna yakini na haki, na mnaifuata, na mnaamini kuwa hakika ndio Yeye Mwenye kuteremsha Qur'ani kuwa ni rehema na uwongofu.
Hapana Mungu isipo kuwa Yeye anaye stahiki kuabudiwa, Yeye peke yake, Mwenye kuhuisha na kufisha. Na Yeye peke yake, ndiye aliye kuumbeni nyinyi na kawaumba baba zenu wa mwanzo.
Basi ewe Mtume! Ngojea ukame utapo wateremkia, wakasibiwa na kukonda na udhaifu wa kuona, ikawa mtu huwa anaona baina ya mbingu na ardhi moshi dhaahiri shaahiri, akawa anasikia mvumo wake wala hauoni.
Watu hawa watawaidhika vipi, hata watimize hiyo Imani wanayo iahidi wakiondolewa adhabu, na hali Mtume mwenye ujumbe ulio wazi kesha wajia na miujiza yenye kuonyesha ukweli wake, na hayo ndiyo mawaidha makubwa kabisa?
Kisha wakaacha kumsadiki Mtume aliye tiliwa nguvu na miujiza iliyo wazi, na wakamwambia: Huo uwongo na uzushi! Mara nyengine wakimsingizia kuwa amefunzwa hayo na mtu, na mara nyengine kuwa akili yake imekorogeka.
Mwenyezi Mungu anawarudi: Sisi hakika tutakuondoleeni adhabu wakati wa duniani, nao ni wakati mchache, lakini nyinyi mtarejea tu, bila ya shaka, yale yale mliyo kuwa mkiyatenda.
Na bila ya shaka tulikwisha wafanyia mtihani, kabla ya makafiri wa Makka, kaumu ya Firauni kwa kuwaitia kwenye Imani, na akawajia Musa, Mtume Mtukufu kwa Mwenyezi Mungu. Wakamkataa kwa inda tu. Na huo ndio mtindo wa hawa washirikina.
Mtume Mtukufu aliwaambia: Nipeni enyi waja wa Mwenyezi Mungu lilio waajibu juu yenu, nalo ni kuitikia wito wangu, kwani mimi ni Mtume nimetumwa makhsusi kwenu, na ni muaminifu katika ujumbe wangu.