Mfano wa yaliyomo katika Sura hii anakufunulia wewe na Mitume walio kuwa kabla yako, Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda kwa nguvu zake, ambaye amepanga kila kitu kwa pahala pake, kwa mujibu wa hikima katika vitendo vyake na mipango yake.
Ni vya Mwenyezi Mungu, peke yake, vyote viliomo katika mbingu na ardhi, kwa kuviumba, kuvimilika, na kuviendesha. Naye ni peke yake aliye tukuka kwa nafsi, na ukawa mkuu ufalme wake.
Mbingu, juu ya ukubwa wake na kushikamana kwake, zimekaribia kupasuka kutoka huko juu kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu, na kuathirika kwa taadhima yake na utukufu wake. Na Malaika wanamtakasa Mwenyezi Mungu na kila lisilo elekea naye, na humsifu kwa analo stahiki. Na humwomba Mwenyezi Mungu awasamehe watu wa duniani. Na Yeye Subhanahu ananabihisha kwamba hakika ni Mwenyezi Mungu tu, peke yake, ndiye Mwenye maghfira ya wote, na rehema iliyo kunjufu.
Na hao walio wafanya wengineo badala ya Mwenyezi Mungu kuwa ndio wa kuwanusuru, Mwenyezi Mungu anaangalia hayo wayatendayo. Wala wewe hukupewa kazi hiyo ya kuwaangalia wao.
Na mfano wa ufunuo huo ulio wazi, tumekufunulia wewe hii Qur'ani kwa lugha ya Kiarabu isiyo na ubabaishi, ili upate kuwaonya watu wa Makka na walio pembezoni mwake katika Waarabu, na uwaonye watu adhabu ya siku watakao kusanywa khalaiki wote kwa ajili ya hisabu. Hapana shaka yoyote kuja siku hiyo. Watu siku hiyo watakuwa mafungu mawili - fungu moja litakuwa Peponi. ma kundi jengine litakuwa Motoni.
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli penda kuwakusanya watu wote katika dunia wakafuata njia moja angeli wakusanya hivyo. Lakini Yeye humtia katika rehema yake amtakaye, kwa kuwa anajua kuwa hao wamekhiari uwongofu kuliko upotofu. Na wenye kujidhulumu nafsi zao kwa ukafiri hawana mlinzi badala ya Mwenyezi Mungu wa kudhamini kuwalinda, wala msaidizi wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Hawa wenye kudhulumu hawakumfanya Mwenyezi Mungu kuwa ni mlinzi wao, bali wamewafanya wengineo kuwa ndio walinzi wao. Na wala haiwafalii wao hayo. Kwani Mwenyezi Mungu, peke yake, ndiye Mwenye kustahiki kuwa Mlinzi kama wao wanataka mlinzi. Yeye ndiye anaye fufua walio kufa kwa ajili ya hisabu. Na Yeye ndiye Mwenye madaraka juu ya kila kitu kwa uweza wake.
Na mliyo khitalifiana kwayo katika mambo yaliyo khusu Imani na ukafiri, hukumu yake ya kukata iko kwa Mwenyezi Mungu. Na Yeye amekwisha ibainisha. Yeye huyo ndiye Hakimu wa kuhukumu mliyo khitalifiana, Mwenyezi Mungu, Mwenye kumiliki mambo yangu yote. Mimi namtegemea Yeye kwa mambo yangu. Na kwake Yeye peke yake ndio narejea ili kutafuta uwongozi.