Ilipo tokea kuwa vikundi viwili vya Waumini kuingiwa na khofu ya kushindwa na wakataka kurejea nyuma, Mwenyezi Mungu aliwalinda akawapa moyo wa kuthibiti, wakasonga mbele katika vita. Kwani hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye utawala katika mambo yao mawili, na ndiye wa kuwalinda na kuwawezesha kwa kuwapa tawfiqi. Basi Waumini nawachukue funzo kutokana na haya, na wamtegemee Yeye ili awanusuru.
Mwenyezi Mungu amewakumbusha Waumini ile neema ya nusura aliyo wapa katika vita vya Badri waliposubiri. Akawahakikishia kuwa Yeye ndiye aliye wapa ushindi katika vita vile na ingawa walikuwa wachache na wapungufu wa silaha; akawataka wamt'ii kuwa ni shukrani kwa neema hiyo. Badri ipo mwendo wa kiasi ya maili 120 kusini magharibi ya Madina. Mpambano hapo baina ya Waislamu na Makureshi ulikuwa siku ya Jumaane 17 Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (13 Machi 624 B.K.). Mtume s.a.w. na Masahaba wake walitoka Madina taarikh 8-9 ya Ramadhani mwaka wa pili wa Hijra (5 Machi 624 B.K.) Idadi ya wapiganaji wa Kiislamu katika vita hivi ilikuwa kiasi watu mia tatu au zaidi kidogo, na Washirikina walizidi mara tatu kuliko hao. Mwenyezi Mungu alitimiza ahadi yake katika vita hivi, Waumini wakashinda juu ya kuwa ni wachache, kwa kuwa Imani yao juu ya haki na uadilifu ilikuwa kubwa. Na kuungwa mkono na Mwenyezi Mungu pamoja na kuwa na moyo wenyewe kulikuwa ni sababu za ushindi kuliko wingi wa watu na ubora wa silaha. Ushindi huu ulio dhaahiri ukawa ndio sababu ya kuenea Neno la Imani na kutukuka likawa juu. Na hichi ni chanzo cha yaliyo kuja baadae, na kivuli cha Uislamu kikatanda Arabuni kote, na kisha kwengineko ulimwenguni.
Ushindi ulipatikana Mtume alipo waambia Waumini: Haitatosha kukutulizeni nafsi zenu Mola wenu Mlezi ikusaidieni kwa Malaika elfu tatu watakao letwa ili kukutieni nguvu?
Ndio! Msaada huo unakutosheni. Na pindi mkivumilia vita, na mkashikilia uchamngu, na hata maadui zenu wakikutokeeni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atawaongeza hao Malaika mpaka wafike elfu tano ili kukupeni nguvu.wakikutokeeni kwa ghafla, Mola wenu Mlezi atawaongeza hao Malaika mpaka wafike elfu tano ili kukupeni nguvu.
Na wala Mwenyezi Mungu hakujaalia huko kukuleteeni msaada wa Malaika ila iwe ni bishara tu kwenu ya ushindi, na zipate kutulia nyoyo zenu. Na hapana ushindi ila unao tokana na Mwenyezi Mungu Mwenye Kushinda wote, ambaye anapanga kila kitu kwa pahala pake, na anaye wapangia mambo waja wake Waumini.
Naye Mwenyezi Mungu amekupeni ushindi ili wateketee baadhi ya wale walio kufuru kwa kuuwawa, au wadhalilike na awakasirishe kwa kushindwa na aibu na hizaya, wapate kurejea nao wameemewa.
Huna lako katika ninayo wafanyia waja wangu, kwani mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Ama atawasamehe kwa Imani, au atawaadhibu kwa kuuwawa na hizaya na mateso ya Siku ya Kiyama, kwani hao ni madhaalimu.
Bila ya shaka vitu vyote vilioko katika Mbingu na katika Ardhi ni vya Mwenyezi Mungu peke yake, kwa kuviumba na kuvimiliki. Na Yeye ndiye Mwenye uwezo juu ya kila kitu, kila kitu kimo mikononi mwake. Yeye humsamehe ampendaye na akamuadhibu amtakaye. Lakini kusamehe kwake ndiko kulio karibu zaidi, na rehema yake ni ya kutarajiwa sana zaidi. Kwani Yeye hakika ni mwingi wa kusamehe na kurehemu.
Enyi mlio amini! Mkikopesha msichukue katika deni ila rasilmali yenu tu. Msifanye kuzidisha juu ya deni faida ya kuzidi mwaka kwa mwaka ikawa kuzidi juu kwa juu. Msiyale mali ya watu kwa upotovu. Hakika nyinyi mtaongokewa na mtafuzu pindi mkiepukana na riba, ikiwa ndogo au kubwa.