Mwenyezi Mungu ni Mmoja, hapana mungu isipo kuwa Yeye. Na kila kiliomo ulimwenguni kinashuhudia hayo kwa namna ya kilivyo umbika na kushikamana, katika umbo na kazi, na viumbe vyenginevyo. Na Yeye Mwenyezi Mungu ni Yuhai, hafi. Ni Mwenye kusimamia na kuendesha mambo yote ya ulimwengu. Yeye ndiye Mwenye kuyadabiri (kuyaendesha) na kuyasarifu.
Umeteremshiwa wewe, Muhammad, hii Qur'ani yenye kukusanya ukweli wa misingi yote ya Sharia ya Mbinguni iliomo katika Vitabu vilivyo tangulia. Na hakika kabla ya Qur'ani Mwenyezi Mungu alikwisha teremsha Taurati kwa Musa, na Injili kwa Isa.
Ameziteremsha hizo kabla ya Qur'ani ili kuwaongoa watu. Walipo kengeuka akaiteremsha Qur'ani ipambanue baina ya Haki na baat'ili, baina ya kweli na uwongo, baina ya uwongofu na upotovu. Basi hii Qur'ani ni Kitabu cha kweli, chenye kudumu milele. Na kila mwenye kuacha aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu na akazikanya Aya zake, Ishara zake, atapata adhabu iliyo kali. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza, hashindwi na kitu, na Mwenye kuwalipa wanao stahiki kulipwa.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu. Kwa hivyo hapana kinacho fichika kwake katika Ardhi na hata katika Mbingu, kikiwa kidogo au kikubwa, kinacho onekana na kisicho onekana.
Ni Yeye, Mwenyezi Mungu, ndiye anakuundeni, anakupeni sura na hali nyinyi mmo matumboni mwa mama zenu, kwa sura na umbo mbali mbali kama apendavyo Yeye. Hapana Mungu ila Yeye Mwenye nguvu katika ufalme wake, Mwenye hikima katika kuunda kwake.
Na Yeye Mwenyezi Mungu ndiye aliye kuteremshia wewe, Muhammad, hii Qur'ani. Na ni katika hikima yake kufanya ndani yake mna Aya zilizo wazi, maana yake na makusudio yake yanajuulikana wepesi. Hizi ndio msingi, ndio asli. Marejeo yote yawe juu ya hizi. Na zipo Aya nyengine za mifano, za mshabaha, zenye kutatanisha. Wengi hawawezi kuzielewa. Na wale ambao hawakubobea, hawakuzama katika ilimu, huwababaisha. Na zimeteremka hizi Aya za mifano ili wanazuoni wachungue kutafuta ilimu ndani yake, na wazingatie, na wazidi kufikiri katika jitihadi, na kufanya uchunguzi katika Dini. Lakini mtindo wa walio iacha Haki ni kutaka kuzifuata hizo Aya za mifano ili kutaka kuchochea fitna, na huzifasiri kwa kufuata matamanio yao. Na hapana anaye jua maana ya Aya hizi kwa hakika ila Mwenyezi Mungu, na wale walio thibiti kweli katika ilimu. Na hao walio thibiti husema: "Sisi tuna yakini kuwa hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu. Sisi hatufarikishi katika kuiamini Qur'ani baina ya sehemu zilizo wazi (Muhkam) na zile za mifano (Mutashaabih). Na hawazingatii ila watu wenye akili iliyo nzima, ambayo haifuati pumbao na matamanio.
Hao wanazuoni wenye akili husema: Mola wetu Mlezi! Usizifanye nyoyo zetu zikaacha Haki baada ya Wewe kwisha tuongoza kuiendea hiyo Haki. Ewe Mola wetu Mlezi! Tupe rehema kutoka kwako kwa kutuwezesha na kututhibitisha. Hakika Wewe ndiwe Mwenye kunyima na ndiwe Mpaji.
Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ndiwe utao wakusanya watu Siku hiyo isiyo na shaka, ili kumlipa kila mmojapo kwa alilo litenda. Kwani Wewe umeahidi hayo, na Wewe hukhalifu miadi yako.