Zakariya a.s. alipo iona neema ya Mwenyezi Mungu kwa Maryamu alimwelekea Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu akimwomba kwa fadhila yake na ukarimu wake na uwezo wake, naye ampe mtoto mwanamume. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maombi ya mwenye kuomba kwake kwa unyenyekevu. Naye ni Muweza wa kuitikia maombi na hata zinge kuwapo pingamizi za kikawaida kama ukongwe na utasa.
Mwenyezi Mungu aliitikia dua yake. Malaika akamnadia naye kasimama pahala pake pa ibada akimwelekea Mola wake Mlezi kumbashiria mtoto mwanamume jina lake Yahya, atakaye muamini Isa a.s. ambaye atazaliwa kwa kauli ya Mwenyezi Mungu kwa njia isiyo ya dasturi. Na Yahya atawahimiza kaumu yake kushika ilimu na kuswali, na atakataza mambo ya pumbao na matamanio, na atamfanya awe miongoni mwa Manabii na watu wema.
Basi Zakariya alipo pewa bishara hii, ya kupata mwana, alimwelekea Mola Mlezi wake kwa shauku ya kutaka kujua vipi yatakuwa hayo, ya kuwa na mwana na ilhali yeye hanazo njia zijuulikanazo, kwa kuwa yeye mwenyewe kesha konga, na mkewe ni tasa. Mwenyezi Mungu akamjibu kuwa Yeye anapo taka jambo ama huzileta njia au huumba bila ya njia zinazo juulikana. Kwani Yeye hutenda apendavyo.
Zakariya akamwomba Mola wake Mlezi amfanyie alama ya kuhakikisha bishara hii. Mwenyezi Mungu akamjibu: Alama yako ni kuwa hutaweza kusema na watu muda wa siku tatu, isipo kuwa utatumia ishara tu kuashiria utakacho. Na shikamana na dhikri ya Mwenyezi Mungu ukimtakasa na kumtukuza jioni na asubuhi.
Na kumbuka ewe Nabii, pale Malaika walipo mwambia Maryamu ya kwamba Mwenyezi Mungu amekukhitari uwe ni mama wa Nabii wake, na amekusafisha na kila uchafu, na amekuteuwa wewe uwe mama wa Isa kuliko wanawake wote wengineo.
Na kwa haya ewe Maryamu, yanakuwajibikia wewe umshukuru Mola wako Mlezi. Basi jilazimishe ut'iifu kwake, na uwe mwenye kushika Swala, na shirikiana na wengine wanao muabudu Mwenyezi Mungu na wanaswali kwa ajili yake.
Haya unayo simuliwa wewe Muhammad na Qur'ani ni katika khabari tukufu za wale alio wateuwa Mwenyezi Mungu, nazo ni khabari za ghaibu ambazo Mwenyezi Mungu anakufunulia. Na wala wewe hukuwapo wakati walipo kuwa wakipiga kura kwa mishale, ili waweze kukata shauri juu ya Maryamu. Na wala wewe hukuwapo walipo gombana kuwania nani wa kupata cheo hicho kitukufu.
Kumbuka na utaje ewe Nabii, pale Malaika walipo mbashiria Maryamu kuwa atamzaa mwana kwa neno lake tu Mwenyezi Mungu kinyume na ada wanavyo zaliwa watu. Jina lake mwana huyo ni Masihi Isa bin Maryamu. Na Mwenyezi Mungu amemjaalia hapa duniani kuwa atakuwa na cheo kwa unabii wake na kuepukana na aibu zote, na kesho Akhera kuwa atakuwa na cheo cha juu pamoja na kundi la walio takasika, wakawa wenye kuwa karibu mno na Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii walio imara baraabara.