Mola wao Mlezi aliwaitikia dua yao, akiwabainishia kuwa Yeye hampotezei mtendaji thawabu za vitendo vyake, sawa sawa akiwa mwanamume au mwanamke, kwani mwanamke anatokana na mwanamume, na mwanamume anatokana na mwanamke. Basi wale walio hajiri, wakahama, wakagura, wanatafuta radhi ya Mwenyezi Mungu, na wakatolewa makwao, na wakapata mateso katika Sabili Llahi, Njia ya Mwenyezi Mungu, wakapigana vita, na wakakhatirisha kuuwawa, bali wakauliwa walio uliwa, Mwenyezi Mungu amejilazimisha Mwenyewe kuwasamehe madhambi yao, na kuwatia kwenye Mabustani yenye kupita kati yake mito, kuwa ni malipo matukufu yaliyo bora kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu peke yake, ndio yako malipo mazuri.
Hizo ni starehe za kupita njia, na kila kipitacho ni duni. Kisha marejeo ya daima watayo ishia ni Jahannamu. Na hapana makaazi maovu kama Jahannamu.
Hayo ndiyo malipo ya makafiri. Ama walio muamini Mwenyezi Mungu wakamwogopa Mola wao Mlezi watapata Mabustani yapitayo mito kati yake, watadumu humo daima, kuwa ni wageni walio pokewa kwa ukarimu na Mwenyezi Mungu, Subhanahu, Aliye takasika. Na yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ndio mazuri kwa watu wema kuliko hayo wanayo starehea makafiri ambayo yataondoka, hayadumu.
Hakika baadhi ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wanamuamini Mwenyezi Mungu, na wanaamini aliyo teremshiwa Nabii Muhammad s.a.w. na walio teremshiwa Mitume walio kuwa kabla yake. Utawaona wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu, na wanakuwa wanyonge kwake, wala hawabadilishi bayana zilizo dhaahiri kwa ajili ya kutafuta pato la duniani. Hilo nalingawa kubwa ni kitu duni. Hawa wana malipo ya ukamilifu kwa Mola wao Mlezi katika makaazi ya kuridhisha. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu, hashindwi kuzidhibiti 'amali zao zote na kuwahisabia. Yeye ni Muweza wa hayo na malipo yake yatawafika bila ya shaka.
Enyi mlio amini! Shikamaneni na subira, na mwashinde maadui zenu katika kusubiri. Na kaeni macho kuilinda mipaka, na mkhofini Mola Mlezi wenu. Katika haya yote ndio mtaraji kufanikiwa. (Jee! Baada ya kuijua Qur'ani yamfalia Muislamu kusema kuwa dini ni kitu mbali na siyasa? Vipi uamrishe mema, ukataze maovu, uhukumu, ukatibiane mikataba na dola nyengine, ukusanye zaka na kuzigawa, upigane Jihadi, ulinde mipaka n.k., n.k. na uiepuke siyasa? Amesema Prof. Khurshid Ahmad: "Uislamu si dini kwa maana ya ovyo ovyo kama lilivyo potoshwa neno hilo, yaani kuwa umemkhusu mtu maisha yake ya binafsi tu. Ni mwendo kaamili wa maisha, unao angalia kila midani ya uhai wa binaadamu. Uislamu ni uwongozi katika kila nyendo za maisha - za binafsi na za jamii, za kimwili na kiroho, za uchumi na siyasa, za sharia na mila, za taifa na za mataifa."--Uislamu, Maana na Ujumbe wake uk. 37)