Kwa sababu ya uasi huo na kupenda kwa baadhi ya watu kuwafanyia uadui wenginewe, ndio tukawajibisha kumuuwa muuwaji, kwani mwenye kumuuwa mtu bila ya sababu zinazo pasa kisasi, au bila ya kufanya uharibifu katika nchi, ni kama amewauwa watu wote. Yeye huyo amemwaga damu za watu, na amewashajiisha wengine wafanye kama hayo. Kwa hivyo kumuuwa mmoja ni kama kuwauwa watu wote kwa kujiletea maudhiko ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Na mwenye kumhuisha mtu kwa kumlipia kisasi, basi ni kama amewahuisha watu wote kwa kuhifadhi damu ya wanaadamu isimwagwe ovyo. Huyo anastahiki thawabu nyingi kutokana na Mola wake Mlezi. Sisi tumewatumia Mitume wetu kutilia mkazo hukumu yetu kwa dalili na hoja. Kisha baadaye wengi miongoni mwa Wana wa Israili walipindukia mipaka katika uharibifu wao katika nchi. Maneno haya yanaonyesha kuwa kumfanyia uadui mtu mmoja ni kuwafanyia jamii ya watu, na kulipa kisasi ndio kuhuisha jamii. Katika Sharia ya Kiislamu kisasi ni haki ya waliy-amri, yaani aliye mkhusu maiti. Akipenda atasamehe achukue fidiya, na akipenda atataka kisasi na akitimize. Naye anapo samehe anayo haki ya kumfedhehesha mkosefu akiwa amekithiri uwovu wake na uharibifu.
Hakika adhabu ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa kuacha hukumu za Sharia, na wakafanya uharibifu katika nchi kwa uharamia na kunyan'ganya mali, ni kuuliwa pindi wakiuwa, na kutundikwa msalabani, pindi wakiuwa na wakapokonya mali ya watu, na kukatwa mikono yao na miguu kwa mabadilisho (yaani mkono wa kulia na mguu wa kushoto, au kinyume cha hayo), pindi ikiwa watavamia watu njiani na kuwapokonya mali bila ya kuwauwa. Na ikiwa watawatisha watu tu, basi adabu yao ni kuhamishwa nchi au wafungwe. Adhabu hizo ni hizaya ya hapa duniani tu, na Akhera watapata adhabu kuu, nayo ni adhabu ya Motoni.
Ila wale walio tubu, miongoni mwa hawa wanao piga vita nidhamu na wakavamia watu majiani, kabla hamjawatia mkononi mkawakamata. Basi adhabu ya Mwenyezi Mungu itaondoka, itabaki juu yao haki za waja wa Mwenyezi Mungu wazirejeshe. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na rehema. Katika hukumu hii inabainishwa kuwa Sharia inaangalia ukhalifu unao athiri jamii, na kwa hivyo adhabu yake ni kali kwa kuwafikiana na kitisho chake kwa wapendao amani. Mazingatio hapa si kwa mujibu wa kile kitendo cha ukhalifu, bali kwa mujibu wa kiasi ya kitisho na fazaa inayo letwa na hicho kitendo.
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu kwa kujitenga na anayo yakataza, na kut'ii amri zake. Na takeni kuyafanya yatakayo kukurubisheni kupata thawabu zake, nayo ni kutenda mambo ya ut'iifu na mambo ya kheri. Na wanieni kwa jihadi katika Njia yake kwa kuitukuza Dini yake na kuwapiga vita maadui zake. Huenda kwa hivyo mkafuzu mkapata karama zake na thawabu zake.
Hakika walio kufuru hata lau kuwa wana kila namna ya mali yote yaliyomo duniani na mambo mengine yanayo onekana yenye maana katika uhai, na wakawa nayo mfano wa yaliyomo duniani juu ya hayo yaliomo humo, na wakataka yawe ni fidiya wajiokoe na adhabu ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama kwa ukafiri wao, basi fidiya hiyo yote haitofaa kitu. Wala Mwenyezi Mungu hawakubalii hayo. Hapana njia yo yote ya wao kuepukana na malipo ya ukafiri wao; nao watapata adhabu kali.