Tradução dos significados do Nobre Qur’an. - Tradução em Swahili - Áli Muhsin

Número de página:close

external-link copy
91 : 5

إِنَّمَا يُرِيدُ ٱلشَّيۡطَٰنُ أَن يُوقِعَ بَيۡنَكُمُ ٱلۡعَدَٰوَةَ وَٱلۡبَغۡضَآءَ فِي ٱلۡخَمۡرِ وَٱلۡمَيۡسِرِ وَيَصُدَّكُمۡ عَن ذِكۡرِ ٱللَّهِ وَعَنِ ٱلصَّلَوٰةِۖ فَهَلۡ أَنتُم مُّنتَهُونَ

Hakika Shet'ani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha? info

Bila ya shaka Shetani hana atakalo kwa kukushawishini kunywa ulevi na kucheza kamari ila kuleta khitilafu na ugomvi na kuchukiana baina yenu ili mdhoofike kwa kuondoka masikizano, na uvunjike umoja wenu, kwa sababu anavyo kukupendeleeni mnywe ulevi na mcheze kamari. Na hayo ili mpate kuacha kumuabudu Mwenyezi Mungu, na muache Swala, ili Akhera yenu iwe ovu kama ilivyo dunia yenu. Basi jee! Baada ya nyinyi kujua maovu haya hamyatupilii mbali ninayo kukutazeni, mkamkosesha Iblisi makusudio yake? Mwenyezi Mungu Mtukufu Aliye takasika ametaja mambo mane yaliyo pelekea kuharimishwa ulevi na kamari: La Kwanza - Kuwa nafsi yake ni uchafu na uovu, kwani hayumkiniki kusifika kuwa ni mambo mazuri, kwa kuwa madhara yake yanaonekana wazi. Katika ulevi kuna uharibifu wa akili, na katika kamari ni kupoteza mali, na kwa yote mawili hayo upo uharibifu wa moyo. Na Shetani ndiye mwenye kuyapamba hayo. La pili - Hayo hueneza uadui na chuki. Kamari humalizikia ugomvi, na kama haifikii hayo basi huleta chuki na bughdha. Na ulevi ndio Mama wa Maasi. Utamwona mtu mwenye adabu zake mpole, akisha kunywa hugeuka nyama mwitu, akatenda mambo ya ukhalifu, kwani ulevi huidhoofisha sauti ya utu inayo mkataza mwanaadamu kutenda maovu. Utamwona mtu anajizuia kufanya kitendo kiovu, lakini akisha kunywa ulevi, au akavuta bangi, japo kidogo, huiendea shari bila ya kujali. Basi si kama ulevi unaharibu akili tu, bali unalaza dhamiri ya mtu. Anakuwa hana junaha. La tatu: Ni kuwa kamari na ulevi huuwa moyo. Mtu huwa hamkumbuki Mwenyezi Mungu, na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndiko kunako huisha nyoyo. Lane: Maasi hayo yanamzuilia mtu na Swala. Kamari na ulevi humsahaulisha Muumini na Swala zake, na akiwa anasali hatimizi nguzo zake kama zitakikanavyo. Basi inakuwa Swala zake ni kuinama na kuinuka bila ya kufuatana na moyo. Kwa hivyo basi imethibiti kuwa kuharimishwa mvinyo, pombe, tembo, bangi n.k. si kwa sababu ya kulevya kwake tu, bali ni kwa kumziba mtu fahamu zake, kumgubika asitambue atendalo. Na kwa hivyo ndio imepokewa kuwa kinacho levya kwa wingi wake, basi hata kidogo chake ni haramu, kwani hicho kidogo nacho kinapumbaza akili. Na juu ya haya pana madhara ya mwili kama madaktari walivyo thibitisha. Kwa hivyo ulevi hata kidogo ni haramu. Mwenyezi Mungu Subhanahu ametaja sababu mbili za kuharimisha ulevi, na udaktari umezidisha kuwa ulevi kidogo haupotezi akili, lakini huzidisha uchangamfu au husabibisha hali ya huzuni na kuona dhiki ya moyo. Na katika hali zote mbili anakuwa mtu amepungukiwa na ukamilifu wa akili yake kubeba jukumu, na kwa hivyo hutenda vitendo ambavyo kwa dhahiri ni sawa kumbe ni madhara. Ama kuuzoea ulevi hudhuru maini, matumbo, na mishipa ya akili na hisiya, na hurithisha madhara mpaka kwa vizazi.

التفاسير:

external-link copy
92 : 5

وَأَطِيعُواْ ٱللَّهَ وَأَطِيعُواْ ٱلرَّسُولَ وَٱحۡذَرُواْۚ فَإِن تَوَلَّيۡتُمۡ فَٱعۡلَمُوٓاْ أَنَّمَا عَلَىٰ رَسُولِنَا ٱلۡبَلَٰغُ ٱلۡمُبِينُ

Na mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, na tahadharini. Na ikiwa mtageuka basi jueni ya kuwa juu ya Mtume wetu ni kufikisha ujumbe tu ulio wazi. info

Na fuateni amri ya Mwenyezi Mungu na amri ya Mtume wake kwa yale anayo kuleteeni kutoka kwa Mola wake Mlezi. Na yaepukeni mbali yatakayo kuleteeni adhabu mnapo kwenda kinyume. Mkitofuata anayo kuamrisheni Mwenyezi Mungu kuweni na yakini kuwa Yeye atakupeni adabu. Wala nyinyi hamna udhuru wowote baada ya kuwa Mtume amekwisha wabainishieni adabu ya kupewa wakhalifu. Na hakika haimpasi Mtume wetu ila kukujuvyeni hukumu zetu tu, na kukubainishieni kwa ukamilifu wa uwazi.

التفاسير:

external-link copy
93 : 5

لَيۡسَ عَلَى ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ جُنَاحٞ فِيمَا طَعِمُوٓاْ إِذَا مَا ٱتَّقَواْ وَّءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّٰلِحَٰتِ ثُمَّ ٱتَّقَواْ وَّءَامَنُواْ ثُمَّ ٱتَّقَواْ وَّأَحۡسَنُواْۚ وَٱللَّهُ يُحِبُّ ٱلۡمُحۡسِنِينَ

Si dhambi juu ya walio amini na wakatenda mema kwa walivyo vila (zamani) maadamu wakichamngu na wakiamini na wakitenda mema, kisha wakachamngu, na wakaamini, kisha wakachamngu na wakafanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri. info

Walio mkubali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda mema, hawana dhambi kwa vyakula vya halali na vizuri wanavyo kula, wala vya haramu walivyo wahi kula zamani kabla hawajajua kuwa ni haramu, ikiwa wanamkhofu Mwenyezi Mungu na wakajitenga navyo vyakula hivyo baada ya kujua kuwa vinakatazwa. Kisha ikawa wao wakaendelea kumkhofu Mwenyezi Mungu na kuzikubali sharia zake, na kisha wakadumu katika khofu yao ya kumwogopa Mwenyezi Mungu katika kila hali, na wakawa wanafanya a'mali zao kwa usafi wa niya, na kwa njia ya ukamilifu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu huwalipa wenye ikhlasi katika vitendo vyao kwa kadri ya ikhlasi yao na a'mali yao.

التفاسير:

external-link copy
94 : 5

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَيَبۡلُوَنَّكُمُ ٱللَّهُ بِشَيۡءٖ مِّنَ ٱلصَّيۡدِ تَنَالُهُۥٓ أَيۡدِيكُمۡ وَرِمَاحُكُمۡ لِيَعۡلَمَ ٱللَّهُ مَن يَخَافُهُۥ بِٱلۡغَيۡبِۚ فَمَنِ ٱعۡتَدَىٰ بَعۡدَ ذَٰلِكَ فَلَهُۥ عَذَابٌ أَلِيمٞ

Enyi mlio amini! Mwenyezi Mungu atakujaribuni kidogo kwa wanyama wa kuwinda inayo wafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue nani anaye mkhofu kwa ghaibu. Basi atakaye ruka mipaka baada ya hayo atapata adhabu kali. info

Enyi mlio amini! Hakika Mwenyezi Mungu anakufanyieni mtihani wakati wa Hija kwa kukuharimishieni baadhi ya wanyama na ndege ambao mnaweza kuwawinda kwa wepesi kwa mikono yenu na mikuki yenu. Makusudio ni kutaka wajuulikane ambao wanamt'ii Mwenyezi Mungu ijapo kuwa hawaonekani na watu. Na wanao pindukia mipaka aliyo iweka Mwenyezi Mungu baada ya kuibainisha watakuja pata adhabu kali.

التفاسير:

external-link copy
95 : 5

يَٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا تَقۡتُلُواْ ٱلصَّيۡدَ وَأَنتُمۡ حُرُمٞۚ وَمَن قَتَلَهُۥ مِنكُم مُّتَعَمِّدٗا فَجَزَآءٞ مِّثۡلُ مَا قَتَلَ مِنَ ٱلنَّعَمِ يَحۡكُمُ بِهِۦ ذَوَا عَدۡلٖ مِّنكُمۡ هَدۡيَۢا بَٰلِغَ ٱلۡكَعۡبَةِ أَوۡ كَفَّٰرَةٞ طَعَامُ مَسَٰكِينَ أَوۡ عَدۡلُ ذَٰلِكَ صِيَامٗا لِّيَذُوقَ وَبَالَ أَمۡرِهِۦۗ عَفَا ٱللَّهُ عَمَّا سَلَفَۚ وَمَنۡ عَادَ فَيَنتَقِمُ ٱللَّهُ مِنۡهُۚ وَٱللَّهُ عَزِيزٞ ذُو ٱنتِقَامٍ

Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyo pita; lakini atakaye fanya tena Mwenyezi Mungu atampa adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu na Mwenye kuadhibu. info

Enyi ambao mmeamini! Msiuwe nyama wa kuwinda nanyi mmenuia Hija na Umra na mmo kuzitimiliza. Na mwenye kumuuwa mnyama kama huyo kwa kukusudia basi itampasa atoe fidiya mfano wa mnyama aliye muuwa, ikiwa katika ngamia, ng'ombe au kondoo. Na hujuulikana huyo mfano wake kwa kukadiriwa na watu wawili waadilifu kati yenu, wahukumu na wawape mafakiri kwenye Al Kaaba, au atoe badala yake awape, au atoe chakula kadiri ya yule mnyama kuwapa mafakiri. Kila fakiri apewe chakula cha kumtosha kutwa yake. Hayo ndio kuondoa dhambi za kuwinda kuliko katazwa. Au badala ya hayo yote, afunge idadi ya siku za kadri ya wale masikini iliyo mbidi kuwalisha lau angewalisha. Na Mwenyezi Mungu amelazimisha hayo ili huyo mwenye kufanya lile kosa apate kuhisi matokeo ya kosa lake na uwovu wa malipo yake. Mwenyezi Mungu, lakini, amesamehe ukhalifu ulio tendekea kabla ya jambo hilo halijaharimishwa. Na mwenye kurejea tena kufanya uovu baada ya kujua kuwa ni haramu, basi hakika Mwenyezi Mungu atampa adabu kwa kitendo chake, naye Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda hashindiki, Mkali wa kumuadhibu anaye kakamia kutenda dhambi. (Tunaona kuwa Uislamu ulianzisha kulinda mazingara, na utajiri wa asili tangu hapo kale. Kutokana na kuhifadhiwa wanyama na ndege wa porini huko Makka, ndio hii leo tunaona zipo nyanda na mapori yanayo hifadhiwa wanyama wake, kwa mujibu wa utaalamu wa kisasa.)

التفاسير: