Na wale wanayo ipinga Dini ya Mwenyezi Mungu, na wakakanusha Ishara zinazo onyesha Umoja wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na ukweli wa Ujumbe wake, hao ni watu wa kudumu katika Jahannamu.
Enyi Waumini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu katika wakati wa shida, pale baadhi ya Washirikina walipo kusudia kukuuweni nyinyi na Mtume wenu, Mwenyezi Mungu akazuia balaa yao isikufikieni, na akakuokoeni. Shikamaneni na kumcha Mwenyezi Mungu, na mumtegemee Yeye peke yake, katika mambo yenu. Kwani Yeye anakutosheni. Inavyo muelekea Muumini ni kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake daima milele.
Mwenyezi Mungu alichukua ahadi kutokana na Wana wa Israili kuwa watamsikia na watamt'ii. Akawateulia marais thinaashara (kumi na mbili) kutokana miongoni mwao ili itimie hiyo ahadi. Na Yeye Mwenyezi Mungu akawaahidi ahadi ya nguvu kuwa atakuwa pamoja nao, atawasaidia na atawanusuru ikiwa watashika Swala kama ipasavyo, na watatoa Zaka walizo faridhiwa, na watawasadiki Mitume wake wote, na watawanusuru, na watatoa mali kwa ajili ya mambo ya kheri. Na kwamba pindi wakifanya hayo basi Mwenyezi Mungu atawafutia dhambi zao, na atawatia katika Bustani zake zipitazo mito kati yake. Na mwenye kukufuru, na akavunja ahadi baada ya hayo, basi huyo amepotoka na hakufuata njia iliyo kaa sawa iliyo nyooka.
Basi kwa sababu ya Wana wa Israili kuvunja agano lao ndio wakastahiki kufukuzwa kutokana na rehema ya Mwenyezi Mungu. Nyoyo zao zikawa ngumu, si laini za kupokea Haki; na wakaingia kupotoa maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyomo katika Taurati kutokana na maana yake ya asli, na yafuate yanayo wafikiana na wapendavyo wao. Wakaachilia mbali pande kubwa ya mambo waliyo amrishwa katika Taurati !! Na wewe, Mtume, huachi kuona kila namna ya khadaa na uvunjaji wa ahadi kwa hawa Wana wa Israili, isipo kuwa kwa wachache tu miongoni mwao ambao wanakuamini wewe. Hao hawakhuni wala hawadanganyi. Basi, ewe Mtume! Yasamehe yaliyo pita kutokana na watu hawa, na wachilia mbali, bali wafanyie wema. Kwani Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.