Na sisi tunasema: Ewe Mola Mlezi wetu! Tumekisadiki Kitabu chako ulicho mteremshia Nabii wako, na tunaifuata amri ya Mtume wako, Isa a.s. Basi tuthibitishe kuwa miongoni mwa wenye kumshuhudia Mtume wako katika kufikisha ujumbe, na kuwashuhudia Wana wa Israili katika ukafiri wao na upinzani wao.
Ama hao makafiri wapinzani walipanga njama za chini kwa chini kuupiga vita wito (Da'wa) wa Isa. Mwenyezi Mungu alizibat'ilisha njama zao, wasifanikiwe kuyapata waliyo yakusudia. Na Mwenyezi Mungu kwa hikima yake anawashinda watu wote wafanyao hila.
Taja ewe Nabii, pale Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa Mimi nitakutimizia ajali yako,(yaani nitakufisha kifo cha kawaida kama alivyo sema Ibn Abbas r.a. Taz. Ibn Kathir) wala sitamwezesha mtu yeyote kukuuwa. Nami nitakunyanyua pahala pa utukufu wangu, na nitakuepusha na maadui wako wanao kusudia kukuuwa, na nitawafanya wanao kufuata wasio kengeuka na dini yako, wawe na nguvu na utawala juu ya wale wasio fuata uwongofu wako, mpaka Siku ya Kiyama. Kisha marejeo yenu ni Akhera. Hapo nitawahukumu katika hayo mlio kuwa mkizozana kwayo katika mambo ya dini.
Ama wale wanao kataa kwa ukafiri nitawaonjesha adhabu ya hizaya na mateso kwa kuwasalitisha mataifa mengine juu yao katika dunia, na hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi na ina hizaya zaidi. Na wala hawana wa kuwaokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na ama walio ongoka kwa uwongofu wa Mwenyezi Mungu, wakatenda vitendo vya kufuata mwendo wa kheri, Mwenyezi Mungu atawapa malipo ya kutosha kwa hizo a'mali zao. Na ndiyo shani yake Mwenyezi Mungu kuwa hawalipi thawabu zake wale wanao pindukia mipaka ya Mwenyezi Mungu wakafanya jeuri ya kutoitikia wito wake na kumtendea wema. Wala hawanyanyulii cheo chao.
Hayo tuliyo kusimulia ni miongoni ya hoja zenye kuonyesha ukweli wa ujumbe wako, nayo ni katika Qur'ani Tukufu yenye kukumbusha, na yenye kukusanya ilimu ya manufaa.
Baadhi ya watu wamepotea katika kadhiya ya Isa, wakadai ati kuwa yeye ni Mwana wa Mwenyezi Mungu kwa kuwa kazaliwa bila ya baba. Mwenyezi Mungu anawaambia: Hakika shani ya Isa katika kuumbwa kwake bila ya baba ni kama shani ya Adam alivyo umbwa kwa udongo bila ya baba wala mama. Mwenyezi Mungu alimfanya na akataka awe, akawa mtu sawasawa.
Bayana hii katika kuumbwa Isa ndiyo ukweli wenyewe ambao unabainisha hakika yaliyo tokea katika khabari za Mola Mlezi wa viumbe vyote. Basi wewe dumu katika yakini yako wala usiwe katika wenye kutia shaka.
Basi wenye kujadiliana nawe, ewe Nabii, katika shani ya Isa baada ya kukujia wewe khabari iliyo toka kwa Mwenyezi Mungu na ambayo haina ubabaifu ndani yake, basi waambie kauli itakayo dhihirisha ujuzi wako wa yakini na upotovu wao wa uwongo: Njooni! Kila mmoja wetu na wenu awaite watoto wake, na wakeze na wenyewe nafsi zao. Kisha tumnyenyekee Mwenyezi Mungu kumtaka ateremshe ghadhabu yake na nakama yake juu ya aliye mwongo katika hili jambo la Isa kuzaliwa bila ya baba na kuwa yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu wala si Mwana wa Mungu.