Basi na watahadhari wale wanao ikhalifu amri yake na Siku ambayo kila mtu atakuta vitendo vyake vya kheri hata kilicho kichache kimeletwa hadharani; na pia uovu wake alio utenda ambao angetamani lau kuwa uko mbali, mwisho wa umbali, hata asiuone kwa kuuchukia na kukhofu kutumbukia katika adhabu zake. Na Mwenyezi Mungu anakuhadharisheni na adhabu zake pindi mkitokana na ulinzi wake na utawala wake, ambao ni upole na rehema kwa waja wake.
Sema: Ikiwa nyinyi ni wakweli katika madai yenu, kuwa mnampenda Mwenyezi Mungu na mnataka Mwenyezi Mungu akupendeni, basi nifuateni mimi kwa ninayo kuamrisheni na ninayo kukatazeni. Kwani mimi nimetumwa na Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu atakupendeni kwa hivyo, na atakulipeni kwa kukufanyieni hisani na kusamehe makosa yenu. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kuwasamehe na kuwarehemu waja wake.
Sema: Mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na wakikukataa basi hao ni makafiri, wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawapendi makafiri.
Kama Mwenyezi Mungu alivyo mteua Muhammad afikishe ujumbe wake, na akajaalia kumfuata Muhammad ni njia ya kufikia mapenzi ya Mwenyezi Mungu na kupata maghfira na rehema yake, kadhaalika ametaja Mwenyezi Mungu kuwa Yeye alimteua Adam na akamjaalia ni katika wateule wa walimwengu. Pia alimteua Nuhu kwa kumpa ujumbe, na akamteua Ibrahim na ukoo wake, nao ni Ismail na Is-haq na Manabii wengine kutokana na wana wao hao. Miongoni mwao ni Musa a.s. Akawakhitari ukoo wa Imran, na miongoni mwao akamkhitari Isa na mama yake. Alimfanya Isa awe ni Mtume kwa Wana wa Israili, na Maryam akamfanya awe ni mama wa Isa bila ya baba.
Amewakhitari hao ukoo ulio safi, wakirithiana usafi na fadhila na kheri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia maneno ya waja wake kwa vitendo vyao na vinavyo fichwa vifuani mwao.
Ewe Nabii! Taja hali ya mke wa Imran alipo weka nadhiri wakati alipo kuwa na mimba, kuwa mwana aliomo tumboni mwake awe ni wa kumtumikia Mwenyezi Mungu tu na kukhudumia nyumba yake. Alisema: Ewe Mola! Hakika mimi nimekuwekea nadhiri huyu aliyomo tumboni mwangu awe ni wa kukhudumia nyumba yako, basi nikubalie haya. Hakika Wewe ni Mwenye kusikia kila kauli, na Mwenye kujua kila hali.
Alipo jifungua mimba akasema kwa kujiudhuru kumwambia Mola wake Mlezi: Niliye mzaa ni mwanamke - na Mwenyezi Mungu anajua vilivyo alicho kizaa, na kuwa mwana wenyewe ni mwanamke ni bora kuliko alivyo taka mama kuwa awe mwanamume. Akasema yule mama: Mimi nimemwita Maryamu, na mimi nakuomba umlinde yeye na ukoo wake na uharibifu wa Shetani maluuni.
Mwenyezi Mungu alimpokea Maryamu kuwa ni nadhiri aliyo iweka mama yake, akamwitikia maombi yake, akamkuza makuzo mema, na akamlea katika kheri yake, Mola Mlezi, huku akimruzuku na kumshughulikia kwa malezi mazuri ya kumpa nguvu mwili wake na roho yake. Mwenyezi Mungu akamkabidhi Zakariya a.s. awe mlezi wake. Zakariya kila akiingia chumbani, alipo kuwa Maryamu anaabudu, akikuta chakula wasicho kizowea wakati ule. Zakariya akasema kwa kustaajabu: Ewe Maryamu! Umepata wapi riziki hii? Naye akamjibu: Hichi ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu. Ni shani yake kumruzuku mja wake amtakaye riziki nyingi bila ya hisabu au kipimo.