Ikawa vumbi la kupeperushwa, Aya hizi tukufu zinaeleza hadi gani vitakuwa vitisho vitavyo uteremkia ulimwengu kitapo fika Kiyama. Na katika vitisho hivyo ni hayo masaibu ya dunia yatakayo athiri ardhi na mat'abaka yake. Kwani hii ardhi tunayo ishi juu ya mgongo wake si yenye kutulia na kukaa sawa kwa utimilivu. Kwani hiyo imeundwa kwa mat'abaka ya majabali yaliyo ingiliana ovyo. Huenda baadhi yao yakateremka yakaachana na mengineyo yaliyo jirani nayo. Na huwa hiyo inayo itwa kupasuka kwa mat'abaka ya ardhi, Geological cleavage kama inavyo tokea katika maeneo kadhaa wa kadhaa. Mpasuko huu ulikuwa na ungali kuwa ndio asili ya chini kabisa ya zilzala, mitetemeko, mikubwa kwa kuathirika na nguvu za kudidimiza na kuvuta zinazo fuatana na mat'abaka ya ardhi yanapo vunjika. Basi mizani ya utulivu ya nguvu hizi inapo geuka kwa kuathirika na mambo mengineyo ya nje huenda zikafunguka nguvu za mtikiso mkubwa ndio ikatokea mitetemeko na mitikisiko ya ardhi, ambayo hubomoa kila kitu kiliopo juu ya ardhi karibu na ilipo anzia hiyo zilzala. Na hapo tena hutokea uharibifu mkubwa mno. Na hayo maelezo ya kisayansi hayageuzi kitu, wala hayako mbali na nadhari ya kidini. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huenda akajaalia sababu za maumbile za kawaida zikajumuika kwa njia tusiyo izoea sisi ili zikiingiliana kwa njia ya kutisha ndio sababu ya kuharibika dunia. Hapo maelezo ya kisayansi yanafuatana na Aya zenye kuonya kwa vitisho hivyo vikuu. Na yote hayo yanatokana kwa Mwenyezi Mungu. Na hutokea kwa idhini yake Mwenyezi Mungu kutimiza hukumu yake katika dunia yetu.
Na walikuwa wakisema kwa kukanusha kurejea tena: Ati tutafufuliwa baada ya kwisha kufa, na baadhi ya miili yetu ikisha kuwa udongo na mengine mifupa iliyo chakaa? Ati sisi tutarudishwa tuwe hai mara ya pili?
Na wala Sisi si wenye kushindwa kukubadilisheni sura zenu, na kuzileta nyengine, na tukakuumbeni katika umbo jengine na sura nyengine msiyo ijua.
Bila ya shaka mmekwisha yakinika kuwa Mwenyezi Mungu alikuumbeni mara ya kwanza, basi je, hamkumbuki kwamba Mwenye kuweza hayo ni Mweza zaidi wa kufanya tena.
Ni nyinyi mnayo yateremsha kutoka mawinguni, au ni Sisi ndio Wenye kuyateremsha kuwa ni rehema juu yenu? Katika Kiarabu limetajwa neno Almuzni. Maana yake ni mawingu yanayo leta mvua. Na kitendo cha kunyesha mvua kinahitajia mambo yaliyo khusiana na hali ya hewa maalumu ambayo mwanaadamu hana mamlaka nayo, au kuyaleta kwa juhudi zake. Kwa mfano zinahitajiwa pepo zinazo kwenda kwa mkondo zilizo baridi juu ya nyengine zilizo za joto, au hali za kuondoka utulivu katika anga. Na watu wamejaribu kuinyesha mvua kwa mawingu yanayo pita kwa njia ya ufundi, lakini juhudi hizo mpaka sasa ni majaribio, na lilio thibiti katika sayansi ni kufuzu kwa majaribio hayo ni kudogo mno, na hata hivyo kunalazimu ziwepo hali maalumu za maumbile zinazo saidia.
Sisi tumeufanya huu moto uwe ni ukumbusho wa Moto wa Jahannamu mtapo uona, na uwe ni manufaa kwa wasafiri wa msitu na nyika, wakinafiika kwa kupikia chakula chao na kuotea moto wakati wa baridi.
Na hakika bila ya shaka hicho ni kiapo kikubwa chenye maana ya kufikia mbali, lau kuwa mnafikiri makusudio yake. Aya mbili hizi zinabainisha hadi ya umuhimu wa kiapo hichi kikubwa. Kwani nyota ni vitu vyenye kutoa mwangaza wenyewe, na nyota ya karibu mno kwetu sisi, nayo ni jua, ni kiasi ya masafa ya miaka 500 ya mwangaza. Na nyota ifuatayo kwa ukaribu iko mbali nasi kwa kiasi cha miaka 4 ya mwangaza takriban. Basi nguvu tunazo zitumia kutokana na jua ndizo zinazo tuwezesha kuishi. Lau kuwa umbali wa jua kutokana na ardhi ni duni ya hivyo au zaidi ya hivyo basi hapana shaka kuwa maisha yangeli kuwa taabu, bali ni muhali. Kadhaalika ukubwa wa nyota unakhitalifiana. Zipo nyota kubwa mno hata ukubwa wake unaweza kukusanya hii ardhi na jua juu ya umbali wao. Vipo vikundi vya nyota vinavyo itwa A'naqiid vinaogelea angani zikivuka Njia ya Maziwa The Milky Way mara kwa mara. Wakati wa kupita kwake zikasadifiana kukutana na kikundi cha jua na zikagongana basi hakika hapo itakuwa ndio maangamizo na kumalizika kwa kweli. Hata ikikaribia nyota moja katika nyota zitokazo kwenye jua basi hayo pia yataleta kuharibika mizani na kupelekea maangamizo na kumalizika ulimwengu. Kwa hivyo basi hakika Ishara za mazingatio na uweza wa Mwenyezi Mungu zinaonekana katika ulimwengu huu alio uumba Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala na akaupanga.
Imo katika ubao ulio hifadhiwa Al-lauhu-lmahfudh, usio karibiwa na yeyote ila Malaika walio karibishwa kwa Mwenyezi Mungu. (Kwa watumiaji Computer wanaweza kukisia kuwa hiyo Al-lauhu-lmahfudh ni kama Disk iliyomo ndani ya Computer na haigusi mtu, na Misahafu tunayo iona, na kuisoma, ni kama yapigwayo chapa kutoka hiyo Disk.)