Mfano wa tulivyo bainisha hoja zetu zi wazi katika tuliyo kwisha wateremshia Mitume. Tumemteremshia Muhammad Qur'ani yote, nayo ni Aya zilizo wazi ili ziwe ni hoja juu ya watu. Na hakika Mwenyezi Mungu humuongoa amtakaye kuwaongoa ili isalimike tabia yake na abaidike mbali na inadi na yanayo sabibisha hayo.
Hakika wanao muamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake wote, na Mayahudi wanao nasibika na Musa, na waabuduo nyota na Malaika, na Wakristo wanao nasibika na Isa, na Majusi wanao abudu moto, na washirikina wanao abudu masanamu..hakika wote hawa Mwenyezi Mungu atakuja wapambanua mbali mbali Siku ya Kiyama kwa kumdhihirisha mwenye haki na aliye potea kati yao. Kwani Yeye anajua vyema vitendo vyote vya viumbe vyake. Na atawalipa kwa vitendo vyao.
Ewe mwenye akili! Hujui kwamba hakika Mwenyezi Mungu vinamnyenyekea na kumt'ii vyote viliomo mbinguni na katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi katika watu wanamuamini Mwenyezi Mungu na wanafuata maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki Pepo? Na wapo wengi miongoni mwao wanao puuza na wala hawamuamini, wala hawayatendi maamrisho yake, na kwa hivyo wanastahiki adhabu na hizaya. Na anaye fukuzwa na Mwenyezi Mungu kutokana na rehema yake basi hawezi yeyote kumhishimu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu. Kwani Yeye hutenda ayapendayo.
Haya ni makundi mawili walio zozana kwa mambo yaliyo mkhusu Mola wao Mlezi, na yanayo mstahiki na yasio mstahiki. Kikundi kimoja kikamuamini na kikundi kingine kikakataa. Basi wale walio kataa na kukufuru Mwenyezi Mungu amewaandalia Siku ya Kiyama moto utao wazunguka na kuwapamba kila upande, kama nguo inavyo upamba mwili. Na kuzidi kuwaadhibu Malaika watawamiminia maji ya moto mno juu ya vichwa vyao!
Kila wakijaribu kutoka Motoni kwa wingi wa machungu na dhiki Malaika watawapiga nayo hayo marungu, na watarudishwa huko huko waliko kuwako. Na watawaambia: Onjeni adhabu ya Moto unao unguza kuwa ni malipo ya ukafiri wenu.
Ama walio amini na wakatenda vitendo vyema, hao bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaingiza kwenye Mabustani yanayo pita mito kati ya majumba yake na miti yake. Humo watastarehe kwa kila namna ya starehe, na Malaika watawapamba vikuku vya mikono vya dhahabu na watawapamba kwa lulu. Ama nguo zao za kawaida zitakuwa za hariri.