Tumemtilia nguvu amri yake katika ardhi, akiendesha humo mambo kwa mazingatio yake na utawala wake. Na tukampa ujuzi mwingi kwa njia ambazo kwazo akiweza kuongoza mambo.
Akenda mpaka akafika pahala mbali huko upande wa magharibi, akalikuta jua kwa linavyo onekana kwa macho kama kwamba linazama pahala penye chemchem ya maji ya moto na matope meusi. Na karibu ya chemchem hii Dhul- Qarnaini aliwakuta watu makafiri. Mwenyezi Mungu akamtia moyoni mwake afanye mojapo ya mambo mawili: Ama awaite kwenye Imani, na hili kwa hakika ni jambo zuri; au awapige vita ikiwa hawakuitikia wito wa Imani.
Dhul-Qarnaini akawatangazia: Katika wao aliye jidhulumu nafsi yake kwa kubakia katika ushirikina, basi amestahiki adhabu ya duniani kutokana naye, na kisha atarejea kwa Mola wake Mlezi. Naye atamuadhibu adhabu kali wasio ijua.
Na ama mwenye kumuitikia, na akamuamini Mola wake Mlezi, na akatenda mema, basi atapata malipo mazuri Akhera, na hapa duniani tunamchukulia kwa upole na wepesi.
Hata akafika linapo chomoza jua, kwa ionekanavyo kwa macho, mwisho wa majenzi. Akawaona watu wanaishi katika ushenzi kabisa. Hawana hata cha kuwasitiri na joto.
Mpaka akafika - katika safari yake ya tatu - pahala mbali baina ya milima miwili mirefu...Na huko akakuta watu ambao hawafahamu wanalo ambiwa ila kwa uzito na mashaka. Hiyo ngome au boma baina ya milima miwili iliyo tajwa katika maelezo ya juu ni milima ya Azarbajan na Arminia, na kauli nyingine ni kaskazini ya mwisho katika jimbo la Turkistan.
Walipo ziona nguvu zake na uwezo wake wakamtaka awasimamishie ngome ya kuwalinda na Juju-wa-maajuju. Nao hao ni watu wanao waonea maya, na wanawafisidia na kuwaharibia nchi yao. Na wao walikuwa watayari wamlipe ujira kwa kazi hiyo.
Akawajibu kwa kuwaambia: Mali na madaraka aliyo nijaalia Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko hayo mnayo taka kunipa. Akaanza kusimamisha hiyo ngome, na akawataka wamsaidie kama wawezavyo kwa watu na zana ili awatimizie wayatakayo.
Akawataka wamkusanyie vipande vya chuma. Wakakusanya kama alivyo taka. Akajenga kwa hivyo ngome ndefu iliyo lingana na kingo za milima hiyo miwili. Kisha akawaamrisha wawashe moto, wakauwasha, mpaka chuma kikayayuka. Tena akamimina juu yake shaba iliyo kwisha yayushwa; ikawa ngome madhubuti, haipitiki.