Na hao Wana wa Israili walidhani hawatapata majaribio, yaani shida za kuwafafanua baina ya walio simama imara na wasio simama imara. Kwa hivyo hawakuweza kustahamili, bali wengi wao walipotea wakawa kama vipofu na viziwi. Wakaiacha Haki, na Mwenyezi Mungu akawapatiliza kwa madhila. Baadae walipo rejea kwa Mwenyezi Mungu na wakatubu, alikubali toba zao, na akawarejeshea utukufu wao. Lakini baadae tena wakaingia katika upotofu, na wakawa kama vipofu na viziwi! Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema, na atashuhudia vitendo vyao, na atawalipa kwavyo.
Wenye kudai kuwa Mwenyezi Mungu yu katika Isa bin Maryam hata akawa yeye Mungu, kama wasemavyo Wakristo hii leo, hakika wamekufuru! Yeye Isa hana dhambi ya haya, kwani hakupata kudai hivyo hata mara moja. Bali yeye aliwaamrisha Wana wa Israili wamsafie imani Mwenyezi Mungu peke yake kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye niumba mimi na nyinyi, na ndiye anaye niendeshea mambo yangu yote, na kwamba kila mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu malipo yake ni kuwa hatoingia Peponi kabisa, bali ataingia Motoni, kwa kuwa amekiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kuvunja mipaka yake hataepuka na adhabu.(Yesu kasema: "Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja." Marko 12.28. "Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe".Yohana 5.30 "Ninapaa kwenda kwa...Mungu wangu naye ni Mungu wenu." Yohana 20.17 )
Haiwi mwenye kudai kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja katika Utatu, kama wadaivyo Wakristo sasa, awe anamuamini Mwenyezi Mungu.!! Na hakika iliyo thibiti ni kuwa hapana mungu ila Mwenyezi Mungu mmoja pekee. Na ikiwa hawa walio potoka hawatoacha itikadi zao potovu, wakarejea kwenye ut'iifu wa Mwenyezi Mungu, hapana budi ila itawasibu adhabu kali. (Biblia inasema kuwa ya kwanza katika Amri Kumi alizo pewa Musa ni: "Usiwe na miungu mingine ila mimi." - Kutoka 20.3. "Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa Bwana ndiye Mungu, hapana ila yeye." - Kumbukumbu la Torati 4.35. Katika Injili ya Yohana 17.3 Yesu anamsemeza Mwenyezi Mungu: "Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.")
Je! Watu hawa hawaziachilii mbali hizo itikadi za uzushi na uwongo, wakarejea kwenye Imani ya Mwenyezi Mungu, na wakaomba wafutiwe dhambi zao walizo zitenda? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkunjufu wa maghfira, Mwingi wa rehema.
Isa bin Maryamu si chochote ila ni mwanaadamu aliye pata neema ya Mwenyezi Mungu kwa kuteuliwa kuwa ni Mtume kama walivyo mtangulia wengi kabla yake. Na Mama yake Isa ni mmoja katika wanawake, aliye jaaliwa kuwa ni mkweli katika kauli yake na mwenye kumuamini Mola wake Mlezi. Na yeye na mwanawe, Isa, walikuwa wana mahitajio yanayo hitajiwa na kila mwanaadamu, kama kula na kunywa, na kwenda haja. Na hizo ni dalili za ubinaadamu wao. Basi hebu zingatia, ewe mwenye kusikia, hali ya hao walio ingia upofu hata hawaoni dalili za Ishara zilizo wazi ambazo amewabainishia Mwenyezi Mungu. Tena zingatia vipi wanaiacha Haki juu ya kuwa ni iwazi kabisa.
Ewe Mtume! Waambie hawa wapotovu: Vipi mnamuabudu mungu asiye weza kukudhuruni kwa lolote mkiacha kumuabudu, wala hawezi kukufaeni kwa lolote mkimuabudu!! Vipi mnaacha kumuabudu Mwenyezi Mungu ambaye Yeye ndiye Mungu Mwenye uweza wa kila kitu, naye ni Mwenye kusikia, na Mwenye ujuzi.
Ewe Mtume! Waambie Watu wa Kitabu, yaani Mayahudi na Wakristo: Mwenyezi Mungu anakukatazeni msivuke mipaka katika itikadi zenu hata mkaingia katika upotovu, mkawafanya baadhi ya viumbe vyake kuwa ni miungu; au mkakanusha ujumbe wa baadhi ya Mitume. Na anakukatazeni kufuata matamanio ya watu walio kutangulieni, walio acha njia ya uwongofu, na wakawazuia watu wengi kuifuata njia hiyo, na wakaendelea katika kuiepuka Njia ya Haki.