Na baada ya hawa Manabii tulimtuma Isa mwana wa Maryamu, naye ni mwenye kufuata njia yao, na kuithibitisha Taurati iliyo mtangulia. Naye tulimteremshia Injili yenye uwongofu kuelekea Haki, na yenye kubainisha hukumu, na tuliiteremsha ili isadikishe Taurati iliyo tangulia, na ndani yake pana uwongofu wa kupelekea Haki, na ni mawaidha kwa wachamngu. (Tazama Injili ya Mathayo 5.17 maneno ya Nabii Isa: "Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.")
Na Sisi tuliwaamrisha wafuasi wa Isa, yaani Watu wa Injili, Wakristo, wahukumu kwa hukumu alizo teremsha Mwenyezi Mungu. Na wasio hukumu kwa mujibu wa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu basi hao wameiacha Sharia ya Mwenyezi Mungu, ni waasi.
Na wewe, ewe Nabii, tumekuteremshia Kitabu kikamilifu, nacho ni Qur'ani, chenye kushikamana na haki katika hukumu zake zote na khabari zake, chenye kuwafikiana na kuthibitisha Vitabu vyetu vilivyo tangulia, na kinavishuhudia kuwa ni Vitabu vya Mwenyezi Mungu, na kinalinda yaliyo sahihi, kwa sababu hii Qur'ani haibadiliki. Basi hukumu baina ya Watu wa Kitabu, Mayahudi na Wakristo, wakikutaka uwahukumu kwa mujibu alivyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Wala katika hukumu yako usifuate matamanio yao na matakwa yao, usije ukapotoka ukaacha Haki iliyo kujia. Kila umma katika nyinyi watu, tumeujaalia kuwa na njia yake ya kuitambua Haki, na njia iliyo wazi ya Dini ya kuifuata. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeli taka angeli kufanyeni nyote kundi moja lililo wafikiana, lenye mwendo mmoja, hazikhitalifiani njia zake za kupita kwa zama zote. Lakini Yeye amekujaalieni hivi ili iwe kama mtihani kwenu katika hizo Sharia alizo kupeni, atambulikane mwenye kut'ii na mwenye kuasi. Basi tumieni fursa hii, na mfanye haraka kuwania kutenda vitendo vya kheri. Kwani marejeo yenu nyote yatakuwa kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Hapo atakwambieni hakika ya hayo mliyo kuwa mkikhitalifiana, na kila mmoja wenu atalipwa kwa a'mali yake.
Na wewe ewe Mtume! Tumekuamrisha uhukumu baina ya watu kwa alivyo teremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matakwa yao katika kuhukumu. Na wahadharishe wasije kukugeuza ukaacha baadhi ya aliyo kuteremshia Mwenyezi Mungu. Pindi wakiipuuza hukumu ya Mwenyezi Mungu na wakataka nyengineyo, basi jua kuwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapatiliza kwa kuwafisidia mambo yao, kwa vile zilivyo kwisha fisidika nafsi zao kwa sababu ya madhambi yao waliyo yatenda kwa kukhalifu hukumu zake na Sharia yake. Kisha atawalipa vitendo vyao vyote huko Akhera. Na hakika watu wengi ni wenye kuziasi hukumu za Sharia. Maneno haya yanatukuza Sharia ya Kiislamu katika kuwahukumu watu. Kwanza inatukuka kwa kuwa ni hukumu ya uadilifu na haifuati mipango ya watu ijapo kuwa ni mipotovu, bali inahukumu juu ya hiyo mipango ya watu kwa kheri na shari. Pili Kanuni huwa katika dola ni moja tu kwa watu wote na mat'abaka yote.
Je, hao wanao kataa amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu wanataka wahukumiwe kwa hukumu ya Kijahiliya, ya kijinga, ya kabla ya kufika Uislamu, kulipo kuwa hapana uadilifu, bali matamanio ya nafsi tu ndiyo yliyo kuwa yakihukumu, na mapendeleo na udanganyifu ndio msingi wa hukumu? Huo ndio mwendo wa watu wa zama za Kijahiliya! Yuko aliye bora kuliko Mwenyezi Mungu kuhukumu watu wenye kuyakinika na Sharia na wenye kunyenyekea Haki? Kwa hakika hao ndio wanao tambua ubora wa hukumu za Mwenyezi Mungu.