Nanyi ikumbukeni Siku ya Kiyama pale Mwenyezi Mungu atapo wakusanya mbele yake Mitume wote akawauliza: Hao kaumu zenu niliyo kutumeni kwao wamekujibuni nini? Waliamini au walikanya? Na hao kaumu wakati huo watakuwa wamehudhuria ili hoja iwe juu yao kwa ushahidi wa Mitume wao wakisema: Hakika sisi hatujui yaliyo tokea baada yetu kwa hao ulio tupeleka kwao. Ni Wewe peke yako ndiye unaye jua hayo, kwa kuwa Wewe ndiye uliye kusanya ujuzi wa vilivyo fichikana kama unavyo jua viliyo dhaahiri.
Na wakati huo, Mwenyezi Mungu atamwambia Isa mwana wa Maryamu miongoni mwa Mitume: Kumbuka neema niliyo kuneemesha wewe na mama yako katika dunia, nilipo kutia nguvu kwa Wahyi,(Ufunuo), na nikakutamkisha nawe ni mtoto mchanga ili kumuondolea tuhuma aliyo tuhumiwa mama yako, kama nilivyo kutamkisha nawe ni mtu mzima kwa ufunuo niliyo kufunulia; na nilipo kuneemesha kwa kukufunza kuandika, na nikakuwezesha kusema na kutenda yaliyo sawa, na nikakufunza Kitabu cha Musa na Injili niliyo kuteremshia wewe, na nikakuwezesha kutenda miujiza asiyo weza mtu mwingine kuitenda, ulipo tengeneza ndege kwa udongo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, ukapuliza akawa ndege aliye hai kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, si kwa uweza wako, na ukamponesha mtoto kipofu, na ukamponesha mkoma kwa idhini na uweza wa Mwenyezi Mungu, na yakawa kwa kupitia mikononi mwako makadara ya kufufuka maiti kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na kudra yake, na pale nilipo wazuia Mayahudi wasikuuwe na kukusalibu nilipo waletea miujiza wapate kuamini, nao baadhi yao walikanya na wakadai kuwa hiyo miujiza si lolote ila ni dhaahiri uchawi tu. (Katika Injili ya Luka inasemwa "Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu." Luka 22.43. Na katika Injili ya Yohana 5.30 Yesu anakiri: "Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.")
Ewe Mtume! Watajie umma wako yaliyo tokea tulipo watia hima kikundi cha alio wataka Isa wamuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake Isa, na wakamuitikia wakawa ndio Wanafunzi wake makhsusi, na wakasema: Tumeamini. Na shuhudia ewe Mola wetu Mlezi, kuwa sisi tumesafi niya zetu, na tunafuata amri zako, yaani Waislamu.
Ewe Nabii! Taja pia yaliyo tokea pale wafuasi wa Isa wenye ikhlasi walipo sema: Ewe Isa bin Maryamu! Hivyo Mola wako Mlezi atakuitikia ukimtaka akuteremshie chakula kutoka mbinguni? Isa akawaambia kuwajibu: Kama nyinyi ni kweli mnamuamini Mwenyezi Mungu, basi mkhofuni Yeye, na fuateni amri zake na makatazo yake. Wala msitafute hoja ila nilizo kuleteeni.
Wakasema: Hakika sisi tunataka kula katika chakula hicho, ili nyoyo zetu zitue kwa kudra ya Mwenyezi Mungu tunayo iamini, na tujue kwa kuona kwa macho ya kuwa hakika ni kweli hayo unayo twambia yanatoka kwake Subhanahu, Aliye takasika, na tupate kutoa ushahidi kwa muujiza huu kwa hao ambao hawakuuona.