Na Mwenyezi Mungu anataka mrejee katika ut'iifu wake, na wale wanao fuata ladha zao, na matamanio yao machafu, miongoni mwa makafiri na waasi, wanataka muwe mbali kabisa na njia ya haki.
Mwenyezi Mungu anataka kukufanyieni wepesi katika kutunga sharia ambazo ndani yake zina sahala na takhfifu kwenu. Kwani hakika Mwenyezi Mungu amemuumba mwanaadamu kiumbe dhaifu katika kupambana na matamanio na maelekeo ya nafsi. Kwa hivyo yanayo mlazimu katika sharia yana wepesi na wasaa. Na hayo kwa fadhila yake na taisiri yake Mwenyezi Mungu ndiyo anayo walazimisha waja wake.
Enyi mlio amini! Msinyang'anyane mali nyinyi kwa nyinyi. Lakini ipo ruhusa kufanya biashara kwa kuridhiana. Wala msijiteketeze kwa kuacha amri za Mola wenu Mlezi. Wala mmoja wenu asimtende uwovu mwenziwe, kwani nyote ni nafsi moja. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye rehema daima kwenu.
Na mwenye kuyatenda aliyo yaharimisha Mwenyezi Mungu kwa uvamizi na kupindukia haki yake, basi tutamtia Motoni ateketee huko. Na hayo ni madogo na mepesi kabisa kwa Mwenyezi Mungu.
Mkiyaachilia mbali madhambi makubwa makubwa anayo kukatazeni Mwenyezi Mungu, tutakusameheni makosa yaliyo duni ya hayo, maadamu mnafanya ukomo wa juhudi yenu kwenda sawa; na tutakuwekeni duniani na Akhera mwahali penye ihsani na hishima kwenu.
Wala haifai wanaume kutamani yale waliyo khusishwa nayo wanawake, wala haiwafalii wanawake kutamani waliyo khusishwa nayo wanaume. Kwani kila kikundi kina sehemu yake kwa mujibu wa tabia ya maumbile ya kazi zinazo wawajibikia, na haki wanazo ongezewa. Basi kila mmoja ajielekeze kutaraji ziada ya fadhila za Mwenyezi Mungu kwa kukuza vipawa alivyo pewa yeye na kutafuta msaada juu ya waajibu ulio juu yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi timamu wa kila kitu, na mtu amepewa namna ya kila kitu kinacho msilihi.
Na wote, wanaume na wanawake, tumewajaalia kuwa wanastahiki urithi wao wa kuwarithi wazazi wawili, na jamaa, na wale ambao mfiliwa amefungamana nao kwa agano ambalo matokeo yake ni kuwa amrithi ijapokuwa si jamaa, na amsaidie pindi anahitajia msaada kuwa ni badala yake. Basi mpeni haki yake kila mwenye haki, wala msipunguze kitu. Hakika Mwenyezi Mungu anakuangalieni kwa kila kitu, na yuko pamoja nanyi, anashuhudia yote myafanyayo.