Mwenyezi Mungu akawakasirikia kwa sababu ya kuvunja agano hili, na kuzikataa ishara za Mwenyezi Mungu, na kwa kuwauwa Manabii kwa dhulma, na kuendelea katika upotovu wao kwa kusema: Nyoyo zetu zimefungwa hazikubali hayo unayo tuitia! Nao hawasemi kweli katika kauli yao hiyo, bali Mwenyezi Mungu amezifuta nyoyo zao kwa ukafiri wao, basi ni wachache tu kati yao wanao amini.
Na Mwenyezi Mungu pia amewaghadhibikia kwa kusema kwao uwongo: Hakika sisi tumemuuwa Masihi Isa bin Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na kweli ya yakini ni kuwa hawakumuuwa kama wanavyo zua. Wala hawakumsulubu kama wanavyo dai. Lakini walifananishiwa, nao wakadhani kuwa wamemuuwa na wamemsalibu. Na hakika walimuuwa na kumsalibu aliye shabihiana naye. Nao wakaja kukhitalifiana baada ya hayo, kuwa aliyeuwawa ni Isa au mtu mwengine? Na wote hao, kwa hakika, wamo katika shaka tu juu ya jambo hilo. Kweli iliyopo ni kuwa hawana ujuzi nayo mambo haya, ila ni dhana tu. Kabisa hawakumuuwa Isa. (Wataalamu wa Biblia mpaka hii leo wamo kuzozana katika jambo hili. Mwenye kuzichungua Injili zinazo kubaliwa na Wakristo ataona kuwa hazina uthibitisho kuwa aliye salibiwa ndiye Yesu, au hata huyo naye alikufa msalabani au la.)
Bali Mwenyezi Mungu alimtukuza kwake, akamwokoa na maadui zake, wasimsalibu na wasimuuwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushinda, hashindiki, ni Mwenye hikima katika vitendo vyake. (Taaurati inayo kubaliwa na Mayahudi na Wakristo imesema kuwa anaye kufa kwa kutundikwa msalabani amelaaniwa. Ndio maana Mayahudi wakawa na hamu wamtundike Nabii Isa ili wathibitishe kuwa huyo si chochote ila ni mlaanifu. Je, Mwenyezi Mungu Mtukufu vipi aachilie jambo hilo liwe kwa Mtume wake?)
Na hapana mmojapo katika Watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo) ila atakuja tambua uhakika wa Isa (kuwa ni Nabii wa kweli wa Mwenyezi Mungu, si mwana haramu, wala si mwana wa Mungu) kabla ya kufa kwake, na kuwa yeye Isa ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na atakuja amini imani ambayo haitomfaa kitu, kwa kuwa wakati wake umekwisha pita. Na Siku ya Kiyama Isa atatoa ushahidi juu yao kuwa yeye alifikisha ujumbe, na kuwa yeye ni mtumwa wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Kwa sababu ya udhalimu wao Mayahudi Mwenyezi Mungu amewapa adabu - amewakataza vyakula mbali mbali vilivyo vizuri, vimekuwa kwao ni haramu, na ilhali kwanza vilikuwa halali kwao. Na kwa udhalimu wao wamewazuia watu wengi wasiingie katika Dini ya Mwenyezi Mungu.
Na kwa sababu ya kupenda kula riba - na Mwenyezi Mungu alikwisha wakataza hayo - na kuchukua mali ya watu kwa njia isiyo ya haki, ndio ikawa adabu ya dini ni kuwazuilia na kula vyakula vilivyo vizuri. Na Mwenyezi Mungu amewawekea hao walio kufuru adhabu yenye kutia machungu.
Lakini walio bobea katika ilimu, yaani wataalamu kweli kweli, miongoni mwa Mayahudi, na Waumini katika umma wako, Ewe Nabii, wanasadiki wahyi ulio funuliwa wewe, na walio letewa Mitume wa kabla yako. Na wanao shika Swala baraabara, na wanatoa Zaka, na wanamuamini Mwenyezi Mungu na kufufuliwa na hisabu, hao Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mema kabisa kwa imani yao na ut'iifu wao.