Siku ambayo madaraka ya nguvu, na uendeshaji mambo usio na ukomo wote, ni wa Mwenyezi Mungu pekee. Siku hiyo ndipo atapo hukumu baina ya waja wake. Walio amini na wakatenda mema watadumu katika Bustani zilizo jaa kila namna ya neema.
Na walio kufuru na wakazikanusha Aya za Qur'ani tulizo mteremshia Muhammad, hao watakuta adhabu ya madhila na fedheha.
Na wenye kuacha nchi zao kwa ajili ya kutukuza shani ya Dini yao wakitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, kisha wakauliwa katika uwanja wa Jihadi, au wakafa vitandani mwao, Mwenyezi Mungu atawalipa malipo mazuri kabisa. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa kutoa thawabu za ukarimu.
Na hakika atawatia katika Pepo kwenye vyeo watavyo ridhika navyo na vitawafurahisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuzijua vyema hali zao, basi atawalipa malipo bora, naye ni Mpole huyasamehe makosa yao madogo madogo ya kuteleza.
Huo ndio mwendo wetu katika kuwalipa watu. Hatuwadhulumu. Na Muumini mwenye kulipiza kisasi kwa aliye mfanyia uovu, na akalipiza kwa kadri ya alivyo tendewa bila ya kuzidisha, kisha yule mkosa akaja kumfanyia uadui tena baada yake, basi hakika Mwenyezi Mungu anatoa ahadi ya nguvu kuwa atamnusuru na kumsaidia yule aliye dhulumiwa. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kumsamehe mwenye kulipiza kama alivyo dhulumiwa. Hamtii makosani kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, basi huyasitiri makosa ya kuteleza ya mja wake mt'iifu, wala hamfedhehi Siku ya Kiyama.
Msaada huo ni mwepesi kwa Mwenyezi Mungu, kwani Yeye ni Muweza wa kila kitu. Na katika Ishara za uwezo wake zilio wazi mbele yenu ni utawala wake juu ya ulimwengu wote. Huzungusha usiku na mchana, pengine huzidi huu au huzidi huu. Inakuwa baadhi ya kiza cha usiku pahala pa mwanga wa mchana. Na pengine huwa kinyume cha hivyo. Naye Subhanahu juu ya uwezo wake husikiliza kauli ya aliye dhulumiwa, na anaviona vitendo vya mwenye kudhulumu. Basi humtia adhabuni.
Huo ndio msaada wa wenye kudhulumiwa unao tokana na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na kutenda kwake katika ulimwengu kama atakavyo bila ya kiwango ni kama muonavyo matokeo yake; na kwa hakika Yeye ndiye Mungu wa Haki ambaye hapana mungu mwenginewe pamoja naye. Na kwamba masanamu wanayo yaabudu washirikina ni uwongo, hayana ukweli, na Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliye tukuka juu ya vyote isipo kuwa Yeye Mwenyewe kwa shani yake, na ni Mkuu wa madaraka.
Ewe mwenye akili! Huzingatii haya yalio kuzunguka uyaonayo kwa macho yenye kuonyesha uwezo wa Mwenyezi Mungu, ukamuabudu Yeye peke yake? Yeye ndiye anaye iteremsha mvua kutoka mawinguni, na ardhi ikageuka rangi ya kijani kibichi kwa mimea inayo chipuka, baada ya kuwa na ukame. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole mno kwa waja wake, na anajua vyema yanayo wanufaisha na kwa hivyo akawatengenezea kwa kudra yake.
Kila kiliomo mbinguni na katika ardhi ni chake Yeye, na kinamtumikia Yeye peke yake, na anakiendesha kama apendavyo. Na Yeye hawahitajii waja wake, bali wao ndio wanao mhitajia Yeye. Na Yeye ndiye anaye stahiki peke yake kuhimidiwa na kusifiwa na viumbe vyote.