Na ziada ya starehe yao humo Peponi ni kuwa Mwenyezi Mungu atawajaalia wawe na kauli njema, na vitendo vizuri vya kusifika. Basi watakuwa wakimtakasa Mwenyezi Mungu na kumtukuza, na watakuwa wenyewe kwa wenyewe wakiamiliana kwa mapenzi na amani.
Hakika wale walio kufuru, yaani walio mkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na pamoja na hayo wakawa mtindo wao kuwazuia watu wasiingie katika Uislamu, na kuwafanyia pingamizi Waumini kuingia kwenye Msikiti Mtakatifu wa Makka - na ilhali Mwenyezi Mungu ameufanya huo ni pahala pa amani kwa watu wote, mkaazi na mpita njia - atawapa watu hao adhabu kali. Na hali kadhaalika kila atakaye kengeuka na Haki, na akatenda udhalimu wowote katika pahala patakatifu, Mwenyezi Mungu atamuadhibu adhabu ya kutia uchungu.
Ewe Nabii! Watajie hawa washirikina wanao dai kuwa ati wanamfuata Ibrahim a.s. na wakaifanya Nyumba Takatifu kuwa ni pahala pa kuwekea masanamu yao; watajie kisa cha Ibrahim na Nyumba Takatifu tulipo mwongoza mpaka pahala pake, na tukamuamrisha aijenge, na tukamwambia: Usinishirikishe Mimi na kitu chochote katika ibada. Na isafishe Nyumba yangu na masanamu na uchafu, ili iwe ni pahala pa makusudi ya mwenye kuizunguka kwa kut'ufu, na mwenye kukaa hapo na akafanya ibada.
Ewe Nabii! Wajuvye watu kwamba hakika Mwenyezi Mungu amewalazimisha wawezao miongoni mwao waijie hii Nyumba. Basi waitikie wito wako, watakujia kwa miguu na kwa kupanda ngamia aliye konda kwa ajili ya safari ya kutoka mbali.
Ili wapate manufaa yao ya Kidini kwa kutekeleza Hija na manufaa ya kiduniani kwa kujuana na ndugu zao Waislamu na kushauriana nao katika mambo ya Dini yao na dunia yao. Nao wataje jina la Mwenyezi Mungu katika Siku ya Idi Kubwa na siku tatu zifwatazo, pale wanapo chinja walio jaaliwa, ikiwa ngamia, au ng'ombe au kondoo na mbuzi. Kuleni mpendacho katika hao, na muwalishe walio patwa na shida na ufakiri.
Tena baada ya hao yawapasa waondoe takataka na uchafu ulio wapata wakati ule wa Ih'ram (yaani kuharimia Hija), nao ni majasho na safari ndefu. Pia waondoe nadhiri walizo mwekea Mwenyezi Mungu, ikiwa wameweka nadhiri yoyote. Na waizunguke kwa kwenda kwa miguu ile Nyumba iliyo jengwa kwa ajili ya ibada ya Mwenyezi Mungu duniani.
Na mwenye kuzishika amri za Mwenyezi Mungu na makatazo yake katika Hija yake kwa kuzitukuza katika nafsi yake, hayo yatakuwa ni kheri yake katika dunia yake na Akhera yake. Na Mwenyezi Mungu amekuhalalishieni kula nyama hoa, (mifugo) yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, ila katika hali mnazo zijua kwa mlivyo kwisha somewa katika Qur'ani, kama vile nyamafu na nyenginezo. Basi epukaneni na kuabudu masanamu, kwani ibada hiyo ni uchafu wa kiakili na kiroho, na haimwelekei mwanaadamu kufanya hivyo. Na epukaneni na kusema uwongo, kumzulia Mwenyezi Mungu au mwanaadamu.