Na makafiri wa Makka wameshikwa na udanganyifu, na hawana wanalo litambua juu ya kuwepo dalili zote hizi. Kwa hivyo ndio wanakuhimiza, wewe Nabii, uwaletee adhabu ulio waahidi. Wanasema hayo kwa upinzani na kejeli. Na hayo hapana shaka yoyote yatawapata, lakini kwa wakati alio uweka Mwenyezi Mungu, ama duniani au Akhera. Naye hendi kinyume na ahadi yake, hata ikipita miaka. Kwani siku moja kwake ni kama miaka elfu mnayo ikadiria na kuihisabu. "Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyo hisabu nyinyi." Qur'ani kwa Aya hii tukufu imeutangulia msafara wa wana sayansi kwa kueleza kuwa zama ni kipimo cha mnasaba, na kwamba fikra ya kuwa zama kwa ulimwengu ni moja kama watu wa zamani walivyo kuwa wakifikiri ni makosa.
Na wengi katika watu wa mijini walikuwa madhaalimu kama wao. Nami nikawapa muhula wala sikuwafanyia haraka kuwaadhibu. Na kisha nikawateremshia hiyo adhabu. Na ni kwangu Mimi tu ndio marejeo ya wote Siku ya Kiyama; na hapo nitawalipa kwa wanayo stahiki. Basi enyi makafiri! Msighurike kwa kuchelewa adhabu kukufikieni.
Ewe Nabii! Waambie hao wanao kanusha, wanao kuhimiza waletewe adhabu: Sio kazi yangu mimi kukulipeni kwa vitendo vyenu. Bali hakika mimi ni mwenye kukuhadharisheni kwa hadhari iliyo wazi kwamba kuna adhabu. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kukuhisabuni na kukulipeni.
Na wale walio muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakatenda vitendo vyema, watapata kutokana na Mwenyezi Mungu kusamehewa dhambi zao walizo ziingia, kama kadhaalika watavyo pata riziki ya ukarimu huko Peponi.
Na wale walio jikukusa nafsi zao katika kuipiga vita Qur'ani kushindana na Waumini na kuwapinga, wakitamani na kudai kwa uwongo, kwamba wao watapata wayatakayo - watu hao watabaki milele katika adhabu ya Motoni.
Ewe Nabii! Usihuzunike kwa hizi hila za makafiri. Yalimpata kama haya kila Mtume katika Mitume wetu, na kila Nabii katika Manabii wetu. Nayo ni kuwa kila wakiwasomea kitu kwa kuwaita waifuate Haki Mashetani wa kibinaadamu walio asi wakiyapinga ili waubat'ilishe Wito, na wawatie shaka watu kwa yale wanayo somewa. Makusudio yao ni kujiingiza kati baina ya Nabii na matamanio yake ya kutaka Wito wake uitikiwe. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa wayatakayo. Na mwishoe Haki ndiyo inayo shinda anapo isimamisha Mwenyezi Mungu sharia yake, na akamnusuru Mtume wake. Na Yeye ndiye Mwenye kuzijua hali za watu na vitimbi vyao, Mwenye hikima katika vitendo vyake. Anaweka kila kitu pahala pake.
Na hakika Mwenyezi Mungu amewawezesha waasi wanao kataa Haki waweze kutumbukiza shakashaka na vikwazo katika Njia ya Wito ili uwe ni mtihani na majaribio kwa watu. Makafiri ambao nyoyo zao zimegeuka mawe, na wanaafiki ambao nyoyo zao zina maradhi, huzidi upotovu kwa kueneza shakashaka hizi na kuziunga mkono. Na si ajabu madhaalimu hawa kusimama msimamo huu, kwani wao wamezama katika upotovu na wamevuka mpaka katika inadi na mfarakano.
Na ili walio pewa ilimu ya sharia na Imani wazidi Imani na kujua kwamba wayasemayo Mitume na Manabii hakika ni kweli iliyo teremka kutokana na Mwenyezi Mungu. Na kwamba Mwenyezi Mungu hakika anawalinda Waumini kwa hima yake kutokana na matatizo yote yanayo wapitikia. Na huwaongoa kwenye maarifa ya Njia Iliyo Nyooka nao wakaifuata.
Na walio kufuru hawatengenei. Bali wanaendelea kuitilia shaka Qur'ani mpaka wafikiwe na mauti, iwafikie adhabu ya Siku isiyo kuwa na kheri kwao wala rehema; nayo ni Siku ya Kiyama.