Ewe Nabii! Usihuzunike kwa hizi hila za makafiri. Yalimpata kama haya kila Mtume katika Mitume wetu, na kila Nabii katika Manabii wetu. Nayo ni kuwa kila wakiwasomea kitu kwa kuwaita waifuate Haki Mashetani wa kibinaadamu walio asi wakiyapinga ili waubat'ilishe Wito, na wawatie shaka watu kwa yale wanayo somewa. Makusudio yao ni kujiingiza kati baina ya Nabii na matamanio yake ya kutaka Wito wake uitikiwe. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa wayatakayo. Na mwishoe Haki ndiyo inayo shinda anapo isimamisha Mwenyezi Mungu sharia yake, na akamnusuru Mtume wake. Na Yeye ndiye Mwenye kuzijua hali za watu na vitimbi vyao, Mwenye hikima katika vitendo vyake. Anaweka kila kitu pahala pake.