Nao wako mbioni kumwendea anaye wita, vichwa vyao vimeelekea juu mbinguni, macho yao hayapepesi hata wakitaka, na nyoyo zao tupu hazina wazo lolote kwa wingi wa khofu.
Ewe Nabii! Waeleze watu khabari za vitisho vya Siku ya Kiyama watapo sema walio zidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi: Mola wetu Mlezi, tuakhirishie adhabu, uturejeshe duniani, na utupe muhula kwa muda mdogo, walau tudiriki kuitikia wito wako wa Tawhidi na kuwafuata Mitume. Nao wataambiwa: Leo ndio mwasema haya? Na mmesahau ya kwamba mliapa nyinyi ya kuwa mkifa neema hizi hazitokuondokeeni mtapo fufuliwa Siku ya Kiyama.
Na mkakaa duniani katika maskani zile zile za wale walio tangulia kuzidhulumu nafsi zao kwa ukafiri na maasi miongoni mwa kaumu zilizo kuwa kabla yenu. Na ikadhihiri kwenu kwa kuona mabaki ya vile tulivyo waadhibu wao, na nyinyi msiwaidhike. Na tukakuelezeni waliyo yafanya wao, na nini kilicho wafika. Nanyi msizingatie.
Na wakapanga hao washirikina njama zao kutaka kuvunja Daa'wa, yaani Wito. Na Mwenyezi Mungu anazijua vyema hila zao. Wala vitimbi vyao haviwezi kuiondoa Sharia iliyo thibiti imara kama milima.
Ewe Mtume! Usidhani kuwa Mwenyezi Mungu atawatupa Mitume wake kwa kwenda kinyume na ahadi aliyo wapa kuwa atawanusuru. Kwani Yeye daima ni Mwenye kushinda, hapana mmoja awezaye kumzuia kwa alitakalo, ni Mkali wa kulipiza kwa anaye mkanya na kumuasi.
Basi Mwenyezi Mungu atalipizia Siku ya Kiyama itapo geuzwa ardhi iwe ardhi nyengine sio hii ya sasa, na mbingu hali kadhaalika zigeuzwe ziwe nyengine, na viumbe watolewe makaburini mwao kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu asiye na mshirika, wala wa kumshinda.
Wanafanyiwa hayo ili Mwenyezi Mungu apate kumlipa kila mmoja wao kwa aliyo yachuma katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu Siku ya Kiyama, wala hapana kitu cha kumshughulisha.
Hii Qur'ani ni Tangazo la kuwanasihi na kuwaonya na kuwakhofisha adhabu ya Mwenyezi Mungu, na ili wajue ya kwamba wakikhofu wakazingatia kuwa hakika hapana mungu ila Mungu Mmoja, na ili wenye akili wakumbuke utukufu wa Mola wao Mlezi, na kwa hivyo wajitenge mbali na yale yatayo waletea hilaki.