Ewe Nabii! Wakumbushe watu wako, huenda wakazingatia, wakati Musa alipo waambia watu wake kwa kufuata amri ya Mola wako Mlezi: Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu kwenu, pale alipo kuvueni kutokana na kaumu ya Firauni, nao wakikupatilizeni kwa adhabu ovu kabisa. Wakikufanyisheni kazi ngumu, wakiwachinja watoto wenu wa kiume, na wakiwaacha wa kike na kuwaweka katika unyonge na udhalili bila ya kuwauwa. Na mateso yote yaliyo tajwa na kuokoka ni mtihani mkubwa unao toka kwa Mwenyezi Mungu, ili upate kudhihiri uwezo wa kusubiri na kushukuru.
Na kumbukeni, enyi Wana wa Israil, pale Mola wenu Mlezi alipo kufunzeni, na akasema: Wallahi! Mkishukuru kwa neema niliyo kupeni ya kukuvueni, na mengineyo, kwa kuthibiti juu ya Imani na ut'iifu, basi hapana shaka nitakuzidishieni neema yangu. Na mkiikanya neema yangu kwa ukafiri na maasi, basi hakika nitakuadhibuni kwa adhabu ya kutia uchungu. Kwani adhabu yangu ni kali kwa wanao kanya.
Na Musa aliwaambia watu wake walipo mpinga na kumkanya: Mkizikanya neema za Mwenyezi Mungu, wala msishukuru kwa Imani na ut'iifu, nyinyi na wote waliomo duniani, basi hakika hayo hayatamdhuru Mwenyezi Mungu chochote. Kwani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, hahitajii shukra za wanao shukuru. Yeye ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa dhati yake, bila ya yeyote kumhimidi.
Je! Haijakufikilieni khabari za walio tangulia kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na A'adi, na Thamud, na kaumu nyenginezo zilizo kuja baada yao, ambao hapana anaye wajua ila Mwenyezi Mungu kwa wingi wao. Hao walijiwa na Mitume wao kwa hoja zilizo wazi kuthibitisha ukweli wao. Na hao wakaweka mikono yao kwenye vinywa vyao, kwa mastaajabu na kukanya. Wakawaambia Mitume: Sisi tunaikataa miujiza na ishara mlizo kuja nazo. Na hakika sisi tuna shaka na hayo mnayo tuitia, mambo ya Imani na Tawhidi, ya kuwa Mungu ni mmoja. Sisi hatukuyakinika na chochote, na tuna shaka nayo!
Mitume wakawaambia watu wao, kwa mastaajabu, kuvunja shaka zao za kuwepo Mwenyezi Mungu na kuwa Yeye ni Mmoja peke yake: Hivyo katika kuwepo Mwenyezi Mungu Mmoja peke yake ipo shaka yoyote, na hali Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi bila ya kuwepo mfano wa kuigiza? Na Yeye anakuiteni apate kukusameheni baadhi ya madhambi mliyo yatenda kabla hamjaamini, na anakuakhirisheni mpaka umalizike muda wenu! Hao watu wakawaambia Mitume wao kwa kuudhi: Nyinyi si chochote ila ni watu tu, wanaadamu, kama sisi. Hamna ubora wowote wa kukufadhilisheni juu yetu hata mpewe Utume. Mnataka kwa huo wito wenu mtuzuie tusiabudu walio kuwa wakiabudu baba zetu! Basi tuleteeni hoja iliyo wazi katika tunazo kwambieni.