Mitume wao wakawaambia: Sisi si chochote ila ni watu kama nyinyi, kama mlivyo sema. Walakini Mwenyezi Mungu huwateua awatakaye miongoni mwa waja wake akawapa Unabii na Utume. Wala hatuna sisi uwezo wa kukuleteeni hoja mnayo taka ila Mwenyezi Mungu apendavyo. Na ni juu ya Mwenyezi Mungu tu peke yake ndio wategemee Waumini, na wamtegemee kwa kustahamilia inda zenu na upinzani wenu.
Na sisi tuna udhuru gani wa kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye aliye tuongoza kila mmoja wetu kwenye njia yake na maelekeo yake aliyo mwekea, na akamlazimisha afuate katika Dini? Na hakika sisi tunatilia mkazo tegemeo letu kwa Mwenyezi Mungu; na hapana shaka tutayavumilia maudhi yenu ya inadi na kutaka miujiza. Na juu ya Mwenyezi Mungu peke yake ndio humtegemea wanao tegemea.
Wakuu wa makafiri majabari wenye madaraka wakaazimia watumie nguvu walipo shindwa wote kupambana kwa hoja na dalili. Wakawaambia Mitume wao: Na liwe moja ya mawili. Ama tukutoeni katika nchi yetu, au muingie katika dini yetu. Mwenyezi Mungu akawafunulia Mitume kwa wahyi: Tutawateketeza hao makafiri kwa dhulma yao!
Na baada ya kuwateketeza tutakuwekeni nyinyi katika ardhi yao. Na huko kuwekwa kwa Waumini ni kweli, hakika, kwa mwenye kukhofu kusimama mbele yangu kwa ajili ya hisabu, na akakhofu ahadi yangu ya adhabu. Kwani mwenye kuingia na khofu huwa mt'iifu.
Hao Mitume waliomba nusura wawashinde hao watu wao wanao wapinga, baada ya kukata tamaa kuwa hawataamini tena. Mwenyezi Mungu aliwanusuru, na wakafuzu, na akakhasiri kila mwenye kiburi, akakataa kumt'ii Mwenyezi Mungu, akawa shadidi wa upinzani. (Haya yaliyo wapata Mitume huwapata watu wa Mungu wote wanao wania Haki hata katika zama zetu. Ushindi wa mwisho daima unakuwa kwa walio wema, hoja kuvumilia na kuendelea na kazi ya Mungu).
Kushindwa kwa hao madhaalimu kunatangulia hapa duniani, na baada yake Akhera ipo adhabu ya Jahannamu. Huko watanyweshwa maji yanayo kirihi kama usaha unao toka kwa watu wa Motoni!
Kunywa kwake ni taklifu, ni kama wanayagugumia, na wala hayeshi kiu, kwani hayumkini kuyaonea tamu kwa ukarihi wake na uchafu wake! Na mtu anakuwa ni kama amezungukwa na mauti kila upande kwa shida ziliopo, na wala huko katika Jahannamu hafi akapumzika na yanayo mfika, bali kila wakati anakuta adhabu nyengine kali zaidi.
Hakika hali za vitendo vya kheri wavifanyavyo makafiri duniani na pato lake, kwa kuwa havikujengwa juu ya msingi wa Imani, hali yake ni kama jivu. Ukaja upepo mkali ukalipeperusha siku ya kimbunga kilipo kaza. Siku ya Kiyama hawapati chochote kutokana na vitendo vyao vya namna hivyo vya duniani. Hayumkini wao kunafiika na chochote kutokana navyo, kwani hivyo havina thawabu, kama mtu mwenye vumbi linalo peperuka katika upepo asilo weza kulikamata. Na watu hawa wapotovu hujiona wenyewe ati kuwa ndio wanafanya mema, na ilhali vitendo vyao viko mbali kabisa na Njia ya Haki.