Musa alipo wakabili kwa wito wake ulio tiliwa nguvu na miujiza iliyo wazi, waliyakanusha waliyo yaona, na wakasema: Haya si chochote ila ni uchawi unao mzulia Mwenyezi Mungu. Na hatukupata kusikia haya unayo tuitia kwa baba zetu wa zamani walio tangulia.
Na Musa alisema kumjibu Firauni na kaumu yake: Mola wangu Mlezi anajua kwa hakika kuwa mimi nimeleta Ishara hizi zenye kuonyesha Haki na Uwongofu kutokana naye Yeye. Basi Yeye ndiye shahidi wangu kwa haya, ikiwa nyinyi mnanikadhibisha. Na Yeye anajua kuwa mwisho mwema ni wetu sisi watu wa Haki. Hakika makafiri hawapati kheri.
Na Firauni alipo shindwa kuhojiana na Musa, na akaendelea na jeuri zake, alisema: Enyi wahishimiwa! Mimi sijui kama yupo mungu wenu mwenginewe isipo kuwa mimi. Na akamuamrisha waziri wake Haman amchomee matufali, na amjengee mnara mrefu apande, ende kumtazama huyo mungu anaye mlingania Musa.
Firauni na majeshi yake wakaendelea wakifanya kiburi katika nchi ya Misri kwa upotovu. Na wakadhani kuwa kabisa hawato fufuliwa Akhera kwa ajili ya hisabu na malipo.
Tukamng'oa Firauni kwenye utawala wake, na tukawavutia taratibu yeye na majeshi yake mpaka baharini, na tukawazamisha na huku tunawatupia sababu ya dhulma yao. Basi zingatia, ewe Muhammad, na uwahadharishe watu wako watazame vipi unakuwa mwisho wa wenye kudhulumu katika dunia yao. Na hakika wewe ni mwenye kusaidiwa kupata ushindi juu yao.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: Na tukawafanya hao ni wenye kuitia watu kwenye ukafiri, ambao khatima yake ni Moto. Na Siku ya Kiyama hawampati wa kuwanusuru na kuwatoa kwenye adhabu.
Na tukawafanya katika dunia hii wenye kupata laana, yaani wenye kutolewa wasiipate rehema yetu; na Siku ya Kiyama watakuwa miongoni mwa walio angamizwa. Na yaliyo simuliwa katika Aya mbili hizi juu yao ni dalili ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Na kwa yakini Mwenyezi Mungu alimteremshia Musa Taurati, baada ya kuwahiliki wakanushao katika kaumu zilizo tangulia, ili iwe nuru ya nyoyo. Kwani nyoyo hizo zilikuwa gizani, haziijui Haki wala uwongozi mwema. Kwani hao walikuwa wakitangatanga tu katika upotovu, na hawaijui njia ya kupatia rehema kwa mwenye kutenda kwa ajili yake, na wakawaidhika kwa yaliyomo katika hiyo Taurati, na wakakimbilia kuzifuata amri, na kuyaacha yaliyo katazwa.