Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma wewe uwafikishie watu wote hii Dini ya Haki, ukiwabashiria Pepo wenye kuamini, na ukiwaonya kwa adhabu ya Moto wanao ikataa hii Dini. Na hapana kaumu yoyote katika kaumu zilizo pita ila walijiwa na mtu kutokana na Mwenyezi Mungu wa kuwahadharisha na adhabu yake.
Na ikiwa kaumu yako wanakukadhibisha wewe basi walio kuwa kabla yao waliwakadhibisha Mitume wao vile vile. Na wao waliwaletea miujiza iliyo wazi, na Maandiko ya Mola Mlezi na Kitabu chenye nuru kwa ajili ya kuwaongoza Njia ya kuokoka duniani na Akhera.
Ewe mwenye akili! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu anayateremsha maji kutoka mbinguni, na kwa maji hayo anatoa mazao yanayo khitalifiana rangi zake? Mengine ni mekundu na manjano, na matamu na machungu, mazuri na mabaya. Na katika milima, ipo milima yenye njia na mistari myeupe na myekundu, yenye kukhitalifiana pia kwa kukoza na kufifia. Ya kustaajabisha kitaalamu katika Aya hii tukufu sio tu kwa kukhitalifiana rangi mbali mbali katika milima, ambazo zinatokana na hizo sehemu za maadini zilizo fanya majabali, kama vile chuma huonyesha rangi yake nyekundu, na manganese na makaa ya mawe huonekana kwa rangi nyeusi, au shaba ambayo hudhihirisha rangi ya kijani n.k. Lakini ya kustaajabisha khasa ni kuunganisha baina ya kutoa matunda ya namna mbali mbali na hali miti yake inanyweshwa maji yale yale, na kuumbwa milima myekundu, na myeupe, na myeusi, na yote yana asli moja kwa kuundwa kwake. Wataalamu wa ilimu za t'abaka za ardhi, Jiolojia, wanaita Magma. Na hii Magma moja inapo chomoza pahala mbali mbali katika ardhi, na penye vina mbali mbali (kwenda chini) katika ardhi kutoka juu basi hupatikana khitilafu katika muundo wake na hukusanyika kwa kurindika kuwa ni milima yenye maadini ya rangi mbali mbali. Na huu basi mwendo wa Mwenyezi Mungu ni mmoja. Kwani hakika asli ni moja, na matawi ndiyo yanakhitalifiana kwa kuonekana. Na katika haya yanapatikana manufaa na faida kwa binaadamu.
Na miongoni mwa watu na wanyama, na mifugo, yaani ngamia, ng'ombe, kondoo na mbuzi, kadhaalika zipo khitilafu katika sura, ukubwa na rangi. Na hawazingatii huu muumbo wa ajabu na wakamwogopa aliye umba ila wanazuoni ambao wanatambua siri ya uumbaji wake. Hakika Mwenyezi Mungu Mwenye kushinda anaogopwa na Waumini, naye ni Mwingi wa kuwafutia madhambi yao wanao rejea kwake. Baada ya kueleza kukhitalifiana matunda, na milima, na watu, na wanyama, na mifugo, inaashiriwa kuwa juu ya khitilafu hizi zinazo onekana baina ya hali hizi zote, upo umoja wa asli. Kwani hayo matunda yanatokana na maji yale yale. Na milima inatokana na Magma moja. Kadhaalika khitilafu za rangi, na watu, na wanyama, na mifugo, hazidhihiri katika tone za manii ambavyo vyote hivyo vimetoka mwanzo wake. Na lau hizo tone zingeli chunguzwa kwa darubini ya Maikroskopu kisingeli onekana kitu cha kuonyesha hizo khitilafu zitazo kuwa. Kwani hizo ni siri zilioko ndani yake katika zinazo itwa Genes (Jiinz). Na labda haya pia yanaonyesha kuwa sifa za kurithi ziliomo katika asli ya mimea, na wanyama, na binaadamu, zinalindwa katika maumbile yake, na hazigeuki kwa tabia ya pahala au chakula.
Hakika wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, kwa kukizingatia na kukitenda, na wakashika Swala kwa mujibu itakikanavyo na wakatoa kwa siri na kwa kuonekana baadhi ya alicho waruzuku Mwenyezi Mungu, wanataraji kwa hayo kufanya na Mwenyezi Mungu biashara isiyo anguka faida yake.
Ili Mwenyezi Mungu awalipe ujira wao, na awazidishie juu yake kutokana na fadhila yake kwa anavyo waongezea mema yao na kuwafutia maovu yao. Yeye ni Msamehevu, Mwingi wa kufutia makosa ya kujikwaa, Mwenye kushukuru, Mwingi wa kushukuru kwa ut'iifu wa waja.