Wala haikufalia kwa Yusuf kuvunja mpango alio mkubalia Mwenyezi Mungu, na kumwachia nduguye atoke mkononi mwake. Kwa hivyo maombi yao hayakumlainisha kitu. Akawajibu jawabu mkato, kwa kuwaambia: Mimi najilinda kwa Mwenyezi Mungu isije nafsi yangu ikadhulumu kwa kumzuia yeyote yule isipo kuwa yule yule tuliye mkuta nayo mali yetu. Tukimchukua mwenginewe kwa kumuadhibu tutakuwa katika hao walio vuka mipaka kwa kumshika asiye na makosa kwa madhambi ya mwovu.
Ilipo katika tamaa yao, wakavunjika moyo kukubaliwa maombi yao, wakenda pembeni peke yao wakishauriana juu ya msimamo wao na baba yao. Ilipo ishia shauri kwa mkubwa wao mwenye kupanga mambo yao, aliwaambia: Haikufalieni kuisahau ahadi ya kiapo mliyo mpa baba yenu ya kuwa mtamhifadhi ndugu yenu mpaka mrudi naye, wala mlivyo fungana naye kabla yake kuwa mtamlinda Yusuf, na hayo mkayavunja! Kwa hivyo mimi nitabaki Misri wala sitotoka ila afahamu baba yetu ukweli wa hali hii, na akaniachilia nirejee kwake, au Mwenyezi Mungu anihukumie kurejea kwa hishima, na akanisahilishia njia kwa sababu yoyote ile. Na Yeye ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
Rejeeni nyinyi kwa baba yenu, na msimulieni kisa chote hichi. Na mwambieni: Mkono wa mwanao ulikunjuka akakiiba kikopo cha mfalme, na kimekutikana katika bahasha yake. Kwa huo wizi wake ndio ameshikwa. Nasi hatukwambii ila tuliyo yaona, na wala sisi hatukuwa tunajua yaliyo fichikana katika hukumu ya Mwenyezi Mungu pale tulipo kutaka nawe ukatupa tumhifadhi na turejee naye kwako kama tulivyo ahidiana na tukafungana. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa uadilifu kuliko mahakimu wote.
Na ikiwa wewe una shaka na haya tunayo kwambia mtume mtu akuletee ushahidi wa watu wa Misri. Na pia wewe mwenyewe waulize wasafiri wenzetu tulio rudi nao, ipate kudhihiri kuwa sisi hatuna lawama. Nasi tunakuhakikishia kuwa sisi ni wakweli katika haya tuyasemayo.
Wakarejea wana walio baki kwa Yaa'qub. Wakamueleza kama alivyo wausia kaka yao mkubwa. Khabari ile ikamtibua huzuni zake, zikazidi kwa kumpoteza mwanawe wa pili. Wala hakutua nafsi yake kwa kuwa wao hawana makosa ya kusabibisha kupotea kwake, naye angali na machungu kwa waliyo mfanyia Yusuf. Akapiga ukelele kwa kuwatuhumu akiwaambia: Niya yenu haikusalimika katika kumhifadhi mwanangu, lakini nafsi zenu zimekuchocheeni mumpoteze kama mlivyo mpoteza nduguye. Lau kuwa nyinyi hamkutoa fatwa ya kuwa mwizi ashikwe afanywe mtumwa kuwa ndiyo adabu ya mwizi huyo Mheshimiwa asingeli mshika mwanangu, wala asingeli baki kaka yenu huko Misri. Lakini mimi sina hila ila kustahamili katika msiba wangu kwa maliwaza mema, huku nikitaraji kwa Mwenyezi Mungu anirudishie wanangu wote. Kwani Yeye ndiye Mwenye ujuzi ulio zunguka hali yangu na hali zao. Na Yeye ndiye Mwenye hikima yenye kushinda, na kwa hiyo ndio hunitendea na hunipangia.
Akadhikika kwa waliyo yasema, akajitenga nao, kashughulika na msiba wake na huzuni kumkosa Yusuf. Macho yake yakafanya kiza kwa wingi wa huzuni, naye akiificha sana. Huzuni kubwa huleta ugonjwa wa macho unao itwa GLOKOMA, na weupe huzidi mpaka mtu mwisho anakuwa kipofu.
Siku zikapita na Yaa'qub kazama katika majonzi yake. Wanawe wakaogopa isije kuwa khatari. Wakamkabili kumtaka apunguze huzuni yake, nao wako baina ya kumwonea huruma na kuchukia kuwa bado yu ngali akimkumbuka Yusuf wakamwambia: Kama hukujipunguzia nafsi yako hapana shaka kumkumbuka Yusuf kutakuzidishia machungu yako yakukondeshe mpaka ukaribie kufa, au ufe khasa!
Maneno yao hayakumuathiri hata chembe. Akawajibu kwa kusema: Mimi sikukushitakieni, wala sikukutakeni mnipunguzie machungu yangu! Mimi sina ila Mwenyezi Mungu tu wa kumnyenyekea na kumshitakia dhiki zangu nzito na nyepesi. Wala siwezi kumficha hayo wala lolote nisilo liweza, kwani mimi natambua wema wake wa kutenda na ukunjufu wa rehema yake, jambo ambalo nyinyi hamlijui!