Na kuwa na imani na Mwenyezi Mungu ndio huhuisha matumaini. Kwa hivyo zile dhiki za moyo hazikuondoka kwa matarajio ya Yaa'qub kumrudia wanawe, na yakamtia katika moyo wake kuwa wangali wahai, na kwamba wakati wa kukutana nao ndio umefika. Akawaamrisha wanawe wende wakawatafute, akawaambia: Enyi wanangu! Rejeeni Misri muwe na kaka yenu, na mumtafute Yusuf na nduguye, muulize khabari zao kwa upole bila ya watu kujua. Wala msikate tamaa kwa Mwenyezi Mungu kuturehemu kwa kuwarudisha. Kwani hawakati tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu isipo kuwa wale wanao kanya.
Nduguze Yusuf walimwitikia baba yao kwa matakwa yake. Wakatoka kwenda Misri, na wakajaribu kukutana na mtawala wake ambaye baadae ikadhihiri kuwa ndiye Yusuf! Walipo ingia kwake walisema: Ewe Mheshimiwa! Sisi na watu wetu tumepata shida ya njaa na madhara ya mwili na nafsi. Na tumekuletea mali chache ndio bidhaa yetu. Nayo ni ya kukataliwa kwa kuwa ni kidogo na mbaya, wala haitoshi kwa hayo tunayo taraji kwako. Lakini sisi tunataraji kwako utupimie kwa ukamilifu na utacho tuzidishia kiwe ni sadaka unayo tupa. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu huwalipa wenye kutoa sadaka thawabu njema kabisa.
Yusuf akaingiwa na huruma ya udugu ambayo inasamehe maovu. Akaanza kuwafunulia khabari zake kwa kuwaambia kwa lawama: Je! Mmejua ule uovu mlio mfanyia Yusuf kwa kumtumbukiza kisimani, na maudhi mlio mfanyia nduguye, mkafanya hayo kwa ujinga ulio kusahaulisheni huruma na udugu?
Kuzinduliwa huku kwa furaha kuliwatambulisha kwamba huyu ndiye Yusuf. Wakamtazama kisha wakasema kwa yakini: Hakika wewe ndiye kweli Yusuf! Na Yusuf mwenye ukarimu aliwaambia kwa kuwakubalia: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufadhili kwa kutuvua kwa salama tusihiliki, na kwa kutupa hadhi na madaraka! Na hayo yamekuwa ni malipo ya Mwenyezi Mungu kwa usafi wangu na wema wangu. Na hakika Mwenyezi Mungu haachi ukapotea ujira wa mtendaji mema na akaendelea nao.
Wakasema: Uliyo sema ni kweli, na tunakuhakikishia kwa kiapo kwamba hapana shaka Mwenyezi Mungu amekutukuza kwa uchamngu, na subira, na sera njema. Na amekupa pia utawala na cheo cha juu. Na sisi hakika tulikuwa wenye kutenda dhambi kwa tuliyo kutendea wewe na nduguyo. Kwa hivyo Mwenyezi Mungu ametudhalilisha kwako, na ametulipa malipo ya wenye kutenda dhambi.
Yule Nabii mtukufu akawajibu kwa kusema: Hapana lawama kwenu leo, wala kusutana. Lenu kutoka kwangu ni msamaha ulio mwema kwa fadhila ya nasaba na haki ya udugu. Na namuomba Mwenyezi Mungu akusameheni na akughufirieni. Na Yeye ndiye Mwenye rehema kuu.
Kisha Yusuf akawauliza khabari za baba yao. Walipo mwambia kuwa hali yake ni mbaya na hawezi kuona kwa wingi wa hamu na majonzi, aliwapa kanzu yake, na akawaambia: Rejeeni kwa baba yangu, na hii kanzu mwekeeni usoni pake. Kwa hivyo atakuwa na yakini kuwa mimi nimo katika salama, na moyo wake utajaa furaha, na Mwenyezi Mungu atamjaalia iwe ni sababa ya kurejea kuona kwake. Hapo tena njooni naye kwangu, na ahali zenu wote pamoja.
Wakaondoka na ile kanzu. Na moyo wa Yaa'qub ulikuwa umezama kungojea nini litalo leta safari ya wanawe. Na Mwenyezi Mungu alikuwa yu pamoja naye katika kungojea huko, ikawa roho yake imeshikamana na roho zao. Basi ule msafara wao ulipo toka nchi ya Misri katika njia yake kumwendea yeye, aliwaambia ahali zake hayo kwa kusema: Mimi naihisi harufu ninayo ipenda ya Yusuf inanijaa. Na lau kuwa sikhofu kwamba mtanituhumu kwa niyasemayo ningeli kwambieni mengi ya Yusuf kuliko hizi hisiya na mawazo.
Wale ahali zake wakamjibu jawabu kali wakiapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa yeye yu ngali kuropokwa kwake na kupiswa kwake kwa uzee! Basi akajitayarisha alivyo jitayarisha kwa mapenzi yake yaliyo pita kiasi ya kumpenda Yusuf, na kuendelea kwake kumkumbuka na kutaraji kukutana naye.