Wala hatukusudii kwa hadithi za uwongofu unazo waeleza kuwa ndio upate malipo au manufaa. Ikiwa hawaongoki hawa usiwahuzunikie. Mwenyezi Mungu atawaongoa watu wengineo. Kwani Sisi hatukuwateremshia wao tu peke yao. Na haya si chochote ila ni mawaidha, na mazingatio kwa kila aliye umbwa na Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi.
Na dalili ni nyingi mno za kuonyesha kuwepo Muumba, na Upweke wake, na Ukamilifu wake, ziliomo katika mbingu na ardhi, ambazo wanaziona watu wako, na wanazipuuza kwa inda, hawataki kuzizingatia.
Na kati yao wapo wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu, wanamkubali kuwa ni Mola Mlezi, na kwamba Yeye ni Muumba wa kila kitu. Lakini imani ya wengi wao haikusimama juu ya msingi madhubuti wa Tawhid! Basi hawaukubali Upweke wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya usafi. Lakini katika nafsi zao umo mchanganyiko wa imani unao wapelekea katika njia za washirikina, mapagani.
Kwani wamechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, wakadhaminika isiwapate adhabu ya kuwagubika kwa nakama yake, kama ilivyo wafanyia walio watangulia kabla yao? Au Kiyama kisiwajie kwa ghafla, kikawatesa nao wameshikamana na ushirikina na ukafiri na kisha mwisho wao uwe Motoni?
Ewe Muhammad! Wazindue mwisho wa uwezo wako, na waonyeshe hadi ya juhudi yako, uwaambie: Huu ndio Mwendo wangu na Njia yangu. Nawaita watu wafuate Njia ya Mwenyezi Mungu. Na mimi nimethibiti katika hili jambo langu, na kadhalika anayaitia hayo kila mwenye kunifuata na akaiamini sharia yangu. Na namtakasa Mwenyezi Mungu Subhanahu na kila kisicho kuwa laiki yake. Wala mimi simshirikishi Yeye na kitu chochote.
Wala Sisi hatukuacha mtindo wetu katika kuwateuwa Mitume tulipo kuteuwa wewe, ewe Nabii! Wala hali ya kaumu yako haikuwa mbali na hali ya kaumu nyengine zilizo tangulia. Kwani hatukuwateuwa Malaika kabla yako, bali tuliwateuwa wanaume wanaadamu katika watu wa mijini, ukawateremkia Ufunuo, yaani Wahyi. Tukawatuma kuwa ni wabashiri na waonyaji. Wenye kuongoka wakawaitikia, na wapotovu wakawafanyia inda! Je, watu wako wameghafilika na kweli hii? Je, wamekalishwa kitako wasiweze kutembea wakaona hao wa kale tulivyo wateketeza duniani? Na mwisho wao ni Motoni; wakaamini wenye kuamini tukawaokoa na tukawanusuru duniani. Na malipo ya Akhera ni bora kwa wenye kumkhofu Mwenyezi Mungu, wasimshirikishe wala wasimuasi. Zimeharibika akili zenu, enyi wakaidi, hata hamwezi kufikiri wala kuzingatia!
Ewe Muhammad! Wala usione nusura yangu inakawia, kwani nusura yangu ipo karibu na hakika inakuja. Na Sisi tuliwatuma kabla yako Mitume, na kwa mujibu wa hikima yetu msaada wetu ulikawilia. Na wao wakawa wanaendelea kukanywa na watu wao, mpaka nafsi zilipo tikisika, wakahisi kukata tamaa, nusura yetu ikawadiriki; tukawaneemesha kwa kuwaokoa na kuwaletea amani wale walio stahili kutaka uwokofu kwetu, nao ni Waumini. Tukawageuzia maovu wale walio tenda dhambi kwa inadi na wakashikilia ushirikina. Wala hapana awezae kuizuia adhabu yetu isiwafikie watu wakosefu.
Na Sisi tumekufunulia tuliyo kufunulia katika visa vya Manabii ili kuuthibitisha moyo wako, na iwe ni hidaya kwa watu wako. Na tumetengeneza mazingatio na waadhi wa kuwanawirisha wenye akili na busara, na wanao tambua kuwa Qur'ani ni haki na kweli. Hizi hazikuwa ni hadithi za kutunga, wala nganu za kuzua. Bali hakika ni kweli na ufunuo, wahyi, wenye kuhakikisha ukweli wa yaliyo pita katika Vitabu vya mbinguni, na walio kuja nayo Mitume wengine! Na zinabainisha yanayo hitaji kufafanuliwa katika mambo ya Dini, na zinaongoa kwendea katika Haki na Njia Iliyo Nyooka, na zinafungua milango ya rehema ya Mwenyezi Mungu ili aongoke mwenye kufuata uwongofu wake, na akawa miongoni mwa Waumini wa kweli.