Nao wanashikilia kutoa Zaka kuwapa wanao stahiki. Kwa hivyo wanakusanya ibada ya mwili na ibada ya mali, na baina ya kujisafisha nafsi na kuyasafisha mali. "Na ambao wanatoa Zaka,": Huu waajibu wa kutoa Zaka unapelekea kujenga mashikamano ya umoja baina ya Waislamu, na kutia katika moyo wa kila mtu kuwa ana jukumu kwa nduguye, anahisi kama anavyo hisi yeye, na anaungulika kama anavyo ungulika yeye. Kwa hivyo ni waajibu wake kufanya awezavyo kumkinga na balaa za kilimwengu, na machungu ya ukosefu. Kwa hivyo fakiri au masikini hatomchukia tajiri, bali wote watahisi kama ni ukoo mmoja unao saidiana na wenye kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu. Wala mwenye deni hakati tamaa kuweza kulipa deni lake lilio bakia ikiwa hana cha kumalizia hilo deni. Wala haianguki chini azma ya mujaahidi anaye pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuinusuru Dini yake na kukomboa nchi yake kwa sababu ya kukosa mali ya kutimizia makusudio yake. Wala msafiri au mgeni mhitaji aliye mbali na mali yake hakosi wa kumkidhia haja zake kwa kumsaidia mpaka afike kwake. Na juu ya haya Zaka ilikuwa ni njia moja katika njia kubwa ulio chukua Uislamu kukombolea mateka na wafungwa na kuondoa utumwa. Na Uislamu umeongeza kutimiza malengo yake ya kijamii kwa ulimwengu mzima ikatupilia mbali chuki zinazo chusha za kidini, na ikatoa ruhusa Zaka wapewe makafiri ikihitajia haja kuwakopesha. Hali kadhaalika hupewa wale wanao itumikia Zaka, kama kuikusanya na kuigawa. Pia waandishi, na wasafiri, na wanao khasiri kwa ajili ya kupatanisha wenye kugombana, na wanao wasaidia Waislamu katika vita. Ama makusudio ya kiuchumi ya Zaka ni kuondoa ufakiri popote ulipo, na kumsaidia kila mwenye haja kama ilivyo kwisha tangulia.
Nao wanajihifadhi nafsi zao wasiingiane na wanawake. "Na ambao wanazilinda tupu zao, isipo kuwa kwa wake zao au kwa iliyo wamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa. Lakini anaye taka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka." Aya hizi zinaambatana na Aya nyengine ziliomo katika Suratun Nur zilio anzia: "Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mpigeni kila mmoja wao bakora mia." Hakika Aya hizi tukufu zilizo tajwa zinaashiria maovu ya katika umma yanayo tokea kwa uzinzi. Ama katika umma ni kuvurugika nasaba ya watoto isijuulikane, ama katika siha ni sehemu mbili. KWANZA ni katika mwili, mfano wa kisonono, tego, AIDS n.k. Kisonono huweza kuzalisha maradhi ya urithi kwa watoto hata huweza kuleta upofu. Ama tego (Syphilis) huenea katika mishipa ya damu na ya hisiya na huweza kuishia wazimu, na pia huenea mpaka kwa vizazi, na huenda mtoto akafa tumboni au akatoka na kilema. Ama maradhi ya AIDS (Ukimwi) hayo ni maafa yasiyo semeka, Mwenyezi Mungu atulinde nayo. PILI ni kuathirika mishipa ya hisiya na akili, kwani uzinzi huweza kuathiri dhamiri ya mtu, na kuadhibika nayo, na hata mwishoe huweza kuingia wazimu.
Isipo kuwa kwa njia ya ndoa ya kisharia, au wenye kumiliki masuria. Hao hawalaumiwi. Zamani utumwa ulikuwa ni jambo la kawaida, na ilikuwa mtu akiweza kuchukua katika wajakazi wake akawafanya kuwa ni wakeze. Na Uislamu ulihalalisha utumwa wa mateka katika vita vilivyo fuata sharia ikiwa maadui nao wanakamata watumwa, basi ilikuwa ni halali kuwatendea wao hali kadhaalika. Ikiwa maadui hawawafanyi mateka kuwa ni watumwa basi ilikuwa haiwafalii Waislamu kuwafanya mateka kuwa ni watumwa.
Mwenye kutaka kuingiliana na mwanamke bila ya kupitia njia hizi mbili, basi huyo amevuka mipaka ya sharia hadi ya kuvuka. Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila walicho pewa kuwa ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na watimize kila ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu. Wasikhuni amana, wala wasivunje ahadi.
Na (hao Waumini) wawe ni wenye kuhifadhi kila walicho pewa kuwa ni amana, ikiwa mali au neno au kitendo au chenginecho, na watimize kila ahadi iliyo baina yao na Mwenyezi Mungu au na watu. Wasikhuni amana, wala wasivunje ahadi.
Yawapasa watu waangalie asli ya kuumbwa kwao; kwani hiyo ni dalili za kuonyesha uwezo wetu zenye kupelekea kumuamini Mwenyezi Mungu, na kuamini kufufuliwa. Kwani Sisi tumemuumba mtu kutokana na asli ya udongo.
Kisha tukaumba vizazi vyake, navyo ni kuwa tulimfanya mtu kwanza tone ya mbegu ya uzazi - yaani maji yenye kila sifa ya uhai wa mwanzo. Tukaiweka kwenye tumbo la uzazi, napo ni pahala pa utulivu palipo lindwa.
Kisha tukaifanya hii mbegu ya manii baada ya kuipandisha na yai la mwanamke kuwa damu. Kisha damu tukaigeuza kuwa kipande cha nyama, kisha tukafanya mafupa, na mafupa tukayavika nyama. Kisha tukatimiza uumbaji wake mwishoe baada ya kuipulizia roho kuwa kiumbe kingine mbali ili kuanza kumjenga. Shani ya Mwenyezi Mungu imetukuka kwa utukufu wake na uwezo wake. Yeye hana mshabaha wake na yeyote katika kuumba kwake na kutengeza kwake na kuanzisha kwake. Kisha hakika nyinyi wanaadamu baada ya haya mambo yenu tuliyo yataja ni wenye kuyaendea mauti bila ya shaka yoyote.
Na hakika Sisi tumeziumba mbingu saba zilizo nyanyuka juu yenu. Ndani yake vipo viumbe ambavyo hatukughafilika navyo. Tunavihifadhi na tunaviendesha. Na Sisi kabisa hatughafiliki na viumbe vyetu vyote. Bali tunavilinda visipotee na kuharibika, na tunavipangia mambo yao yote kwa hikima. "Na kwa yakini tumeziumba juu yenu njia saba. Nasi hatukuwa wenye kughafilika na viumbe." Hizo njia saba zilizo tajwa katika hiyo Aya maana yake ni mbingu saba, na kwamba hizo si mbingu moja, na Mwenyezi Mungu haghafiliki na mbingu hizo na viumbe viliomo ndani yake.