Hakika ibada zinazo fanywa usiku zinaganda zaidi katika moyo wa mtu, na zinabainika zaidi ulimini, na zinasibu vyema zaidi, kuliko visomo vya ibada za mchana.
Hakika mchana unakuwa na mambo mengi ya kukuhangaisha kutafuta maslaha ya maisha yako, na kushughulika na mambo ya kufikisha Ujumbe. Basi jiwekee nafsi yako faragha ya usiku kwa ajili ya kumuabudu Mola wako Mlezi.
Yeye ndiye Mwenye kumiliki mashariki na magharibi, hapana wa kuabudiwa kwa haki isipo kuwa Yeye. Basi mfanye Yeye tu ndiye wa kukutosha katika mambo yako yote, ndiye wa kutegemewa peke yake kama alivyo ahidi.
Siku itakapo tikisika ardhi na milima kwa mtikiso mkubwa mno, na milima ikawa mirundu ya mchanga ulio tapanyika, baada ya kuwa mawe magumu yaliyo shikamana.
Enyi watu wa Makka! Hakika Sisi tumekutumieni Muhammad kuwa ni Mtume wa kukushuhudilieni Siku ya Kiyama kwa kukubali na kukataa, kama tulivyo mtuma Musa kwa Firauni awe ni Mtume.
Basi mkikufuru mtajikinga vipi na adhabu ya Siku ambayo kwa kitisho chake itawafanya vijana wawe vikongwe wasio na nguvu?
Mbingu juu ya nguvu zake na ukubwa wake, Siku hiyo zitapasukilia mbali kwa shida zake na vitisho vyake. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni lazima itokee, hapana hivi wala hivi.
Hakika Aya hizi zinazo taja ahadi ya Mwenyezi Mungu ni mawaidha. Kwa hivyo mwenye kutaka kunafiika kwazo ataishika njia ya kumwendea Mola wake Mlezi kwa kuchamngu na kunyenyekea.
Hakika Mola wako Mlezi anajua kwamba wewe, Muhammad, unakesha pengine akali kuliko thuluthi mbili za usiku, na mara nyengine unakesha nusu ya usiku, na pia wanakesha baadhi ya masahaba zako kama ukeshavyo wewe. Na hapana anaye weza kuukadiria urefu wa usiku na mchana, na kudhibiti saa zake, ila Mwenyezi Mungu. Yeye anajua kuwa hamwezi kuhisabu baraabara kila sehemu katika sehemu za usiku na mchana. Kwa hivyo amekukhafifishieni. Basi someni katika Swala kilicho chepesi katika Qur'ani. Yeye anajua kuwa watakuwepo kati yenu walio wagonjwa, ambao watapata taabu kukesha usiku; na wengine wamo safarini kwa ajili ya biashara na kazi, wakitafuta riziki ya Mwenyezi Mungu. Na wengine wanapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kulitukuza Neno lake. Basi someni kilicho chepesi katika Qur'ani, na zishikeni baraabara faridha za Swala, na toeni Zaka iliyo kuwajibikieni, na mkopesheni Mwenyezi Mungu mkopo mwema, kwa kuwapa mafakiri kwa khiari juu ya hayo yaliyo kulazimuni. Na chochote cha kheri mnacho kitanguliza kwa ajili ya nafsi zenu, mtakuta thawabu zake kwa Mwenyezi Mungu zimekuwa bora zaidi kuliko hicho mlicho kiacha na kukitoa, na malipo mema zaidi. Na mtakeni msamaha Mwenyezi Mungu kwa vitendo viovu na kwa upungufu katika vitendo vyema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe madhambi ya Waumini, na ni Mwenye kuwarehemu.