Na hawa wanaafiki walikwisha tangulia kuleta fitna baina yenu, na wewe, ewe Mtume, wakakupangia njama. Lakini Mwenyezi Mungu aliviviza vitimbi vyao, na akahakikisha kukunusuru, na akaipa ushindi Dini yake wao wakipenda wasipende.
Na baadhi ya wanaafiki walikuwa wakimwambia Mtume: Tupe ruhusa tukae tusende kwenye Jihadi, wala usitutie kwenye shida na dhiki. Na wao kwa hakika kwa msimamo huo wamekwisha jitia wenyewe katika maasia, kumuasi Mwenyezi Mungu. Na hakika Siku ya Akhera Moto wa Jahannamu utawazunguka.
Hawa wanaafiki hawakutakii wewe Mtume na Masahaba zako ila mambo ya karaha tu. Wanaona uchungu mkipata kheri yoyote, ikiwa ya ushindi au ngawira; na wanafurahi mkisibiwa na shari, kama kujeruhiwa au kuuwawa! Na yakikupateni hayo wao husema kwa kufurahia msiba wenu: Sisi tulichukua hadhari yetu, kwa kubaki nyuma tusitoke kwenda kwenye Jihadi. Na huenda zao nao wamefurahi.
Waambie ewe Mtume: Hayatupati ya kheri wala ya shari katika hii dunia yetu, ila aliyo tukadiria Mwenyezi Mungu. Kwani sisi turadhi na hukumu ya Mwenyezi Mungu. Hatujitapi kwa kheri, wala hatuingiwi na dukuduku la roho kwa kufikiwa na shari. Hakika Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kuyatawala mambo yetu yote, na juu yake Yeye tu ndio Waumini wa kweli wanategemea.
Ewe Mtume! Waambie hao: Nyinyi msitaraji yatatutufikia sisi ila moja ya mema mawili, ama tushinde na tupate ngawira, au tufe mashahidi katika Njia ya Mwenyezi Mungu na tuingie Peponi kesho Akhera. Na sisi tunakutarajieni ikufikieni adhabu itokayo kwa Mwenyezi Mungu ikuangamizeni; au akuadhibuni kwa udhalili kutokana na mikono yetu. Basi ingojeeni amri ya Mwenyezi Mungu; na sisi pia tunaingoja amri yake pamoja nanyi.
Ewe Mtume! Waambie hao wanaafiki wanao taka kuficha unaafiki wao kwa kutoa michango ya mali kwa ajili ya Jihadi na mengineyo: Toeni mtakacho, kwa khiari au kwa nguvu; Mwenyezi Mungu havikubali vitendo vyenu vilivyo kwisha haribiwa na unaafiki wenu! Kwani nyinyi daima ni wenye kuiasi Dini ya Mwenyezi Mungu, wenye kuipinga amri yake.
Wala Mwenyezi Mungu hakukataza visipokelewe wanavyo vitoa ila kwa kuwa wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ukafiri, kukataa, kunavunja a'mali zote. Na vile kwa kuwa wao hawaswali kwa namna walio amrishwa; kwani wao huswali bila ya kuiamini Swala, ila wanafanya kama ni kuficha unaafiki wao. Wala wao hawatoi kitu isipo kuwa na huku wanachukia huko kutoa ndani ya nyoyo zao.