Na hao Mwenyezi Mungu Mtukufu anawabashiria rehema kunjufu itakayo waenea, na atawakhusisha radhi zake, na hayo ndiyo malipo makuu. Na Siku ya Kiyama atawatia katika Mabustani, na humo watapata neema zenye kuthibiti na kudumu.
Enyi Waumini! Msiwafanye baba zenu, na watoto wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na wake zenu, ndio wasaidizi wenu wa kukunusuruni maadamu wanapenda ukafiri, na wanaufadhilisha kuliko Imani. Na wenye kutaka manusura kwa makafiri, ndio hao walio iwacha Njia Iliyo Nyooka.
Ewe Mtume! Waambie Waumini: Ikiwa baba zenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyo yachuma, na biashara mnazo khofu zisibwage, na majumba mnayo starehea kuyakaa, mnayapenda zaidi kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume na Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, hata mkaacha kumuunga mkono Mtume, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu akuleteeni hukumu yake na adhabu yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi wenye kutoka kwenye mipaka ya Dini yake.
Hakika Mwenyezi Mungu amekunusuruni na maadui zenu mara nyingi katika vita kwa nguvu ya Imani yenu. Na mlipo ghurika na wingi wenu katika vita vya Hunayni, kwanza Mwenyezi Mungu alikuachieni wenyewe. Wingi wenu usikufaeni kitu. Adui akakushindeni, na kwa shida ya kufazaika mkaiona ardhi kuwa ni nyembamba. Msiweze kupata njia ya kupigana wala kuokoka kwa murwa. Wengi wenu wakawa hawana njia ya kuepuka ila kukimbia. Mkakimbia kwa kushindwa, na mkamuacha Mtume na Waumini wachache tu. Vita vya Hunayni walipigana Waislamu na kabila mbili za Thaqiif na Hawaazin. Jeshi la Waislamu lilifika kiasi ya watu elfu kumi na mbili, na makafiri walikuwa elfu nne. Nao walipigana kwa ukali kwa kuwa ilikuwa wakishindwa wao basi ibada ya masanamu itatoweka kabisa kwa Waarabu, kwani Makka ilikuwa ndio kwanza kwisha tekwa. Majeshi mawili yakapambana, Waumini kwa wingi wao, nao uliwapandisha kichwa; na wale makafiri na uchache wao wakali. Kwanza makafiri wakashinda kwa kuwa Waislamu walighurika kwa wingi wao wakajiona. Lakini mwishoe vita vikaishia kwa kushinda Waumini. Funzo la hapa ni kuwa wingi sio unao pelekea ushindi, lakini nguvu za kimoyo na imani.
Tena mkapata himaya ya Mwenyezi Mungu. Akateremsha utulivu juu ya Mtume wake, na akaujaza utulivu katika nyoyo za Waumini, na akakuungeni mkono kwa Malaika, jeshi lake, walio tia imara miguu yenu. Nanyi hamkuwaona Malaika hao...Na Mwenyezi Mungu akawaonjesha maadui zenu machungu ya kushindwa. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri duniani.