Katika Watu wa Kitabu wapo ambao huzipindua ndimi zao kutamka maneno yasiyo kuwamo katika Kitabu kwa lafdhi ya Kitabu, watu wadhanie kuwa ni maneno yanayo toka kwa Mwenyezi Mungu, na wala hayamo katika ufunuo wa Mwenyezi Mungu. Wanamzulia Mwenyezi Mungu nao ndani ya nafsi zao wanajua kuwa wanasema uwongo.
Si akili wala haimfalii mwanaadamu aliye teremshiwa Kitabu na Mwenyezi Mungu na akapewa ilimu ya manufaa na kuweza kuzungumza mambo yanayo tokana na Mwenyezi Mungu, tena awatake watu wamuabudu yeye badala ya kumuabudu Mwenyezi Mungu. Lakini linalo ingia akilini, na lifaalo, ni kuwa yeye awatake watu wamsafie ibada Mola wao Mlezi aliye waumba kwa mujibu alivyo wafunza kutokana na ilimu ya Kitabu na kwa mujibu ya wanayo soma.
Wala hayumkini akuamrisheni kuwafanya Malaika au Manabii kuwa ndio miungu badala ya Mwenyezi Mungu. Ni ukafiri usio ingia akilini kukuamrisheni hayo baada ya kuwa mmekwisha kuwa Waislamu mlio muelekezea nyuso Mwenyezi Mungu. (Nabii Isa a.s. hakujidaia Ungu hata katika Injili hizi zilizo korogwa, wala hakumfanya Roho Mtakatifu, ambaye ni Malaika, kuwa ni Mungu.)
Ewe Nabii! Watajie kuwa Mwenyezi Mungu aliahidiana na akaagana na kila Nabii aliye teremshiwa Kitabu na akapewa ilimu ya manufaa, ya kwamba akija Mtume ambaye wito wake unakubaliana na wito wao basi ni waajibu wao wamuamini na wamsaidie. Na Manabii wote walikiri kuitimiza ahadi hiyo, na wakakiri na wakashuhudia kwa nafsi zao, na Mwenyezi Mungu akawashuhudia hayo. Tena wao wakayafikisha hayo kwa kaumu zao. Ahadi hiyo imewapasia wao imani na wamnusuru wakimwahi. Kama hawakumwahi basi ni waajibu wa kaumu zao wamuamini na wamnusuru kwa kutimiza na kufuata yaliyo walazimu Manabii wao.(Tazama katika Biblia: Kumbukumbu 18.17-19, Injili ya Yohana 16.7-14)
Anaye kataa kumuamini Nabii huyu baada ya ahadi hii madhubuti ni mpotovu aliye toka kwenye sharia ya Mwenyezi Mungu, ni kafiri mwenye kuwakataa Manabii wote wa mwanzo mpaka wa mwisho.
Je, wanataka Dini isiyo kuwa Dini ya Muhammad, na hiyo ndiyo Dini ya Manabii wote? Dini hii ndiyo pekee Dini ya Mwenyezi Mungu anaye nyenyekewa na kila kilichomo mbinguni na duniani kwa ut'iifu, kwa kupenda na khiari, au kwa lazima kwa kufuata tabia na maumbile. Na kwake Yeye ndio viumbe vyote vinarejea.