Enyi Watu wa Kitabu! Kwa nini mkachukua Haki waliyo kuja nayo Manabii, na ikateremshiwa Vitabu, mkaichanganya na mambo ya udanganyifu ya kubuni na mkaleta tafsiri potovu, na msieneze Haki safi iliyo wazi isiyo kuwa na mchanganyiko? Na nyinyi mwajua vyema kuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kitendo kama hichi ni kubwa.
Katika mtindo wao wa kutaka kuwapotoa Waumini, hawa Watu wa Kitabu wakiwaambia wenzao: Jitieni kuiamini Qur'ani aliyo teremshiwa Muhammad asubuhi, na ikifika jioni ikataeni. Huenda kwa hivyo mkawafitini hawa kwa kuwaingiza shaka katika nyoyo zao, wakaiacha dini yao.
Aidha wao husema: Msiwakubalie ila aliye fuata dini yenu, asije yeyote kati yao akadai kuwa nao wamepewa kama mlio pewa nyinyi, au akachukulia hoja mbele ya Mola wenu Mlezi kwa kuwakubalia kwenu. Ewe Nabii! Waambie: Hakika uwongofu wote unateremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye anaye mmiminia na kumteua amtakaye. Na ewe Nabii! Waambie: Hakika fadhila ziko kwa Mwenyezi Mungu humpa amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mkunjufu wa fadhila, Mjuzi wa anaye stahiki hayo na anaye teremkiwa na hayo.
Yeye Mwenyezi Mungu humpa amtakaye Unabii na Utume, na anaye mkhusisha kwa kumpa hayo ni katika fadhila yake tu. Na Mwenyezi Mungu ana fadhila kubwa kubwa kabisa, na wala hapana anaye muingilia yeyote, wala hapana anaye mzuia katika kutoa kwake.
Huo ndio mwendo wao Watu wa Biblia katika itikadi, ama mwendo wao katika mambo ya mali utaona: Kati yao kuna ambaye ukimpa amana ya chungu ya dhahabu au fedha atakurejeshea sawa sawa bila ya kupunguka chochote. Na mwengine kati yao ukimpa amana ya dinari moja tu hakurudushii, ila ikiwa utamshikilia mpaka aitoe. Haya ni kwa sababu wapo baadhi yao wanawaona watu wa mataifa mengine, si watu wa Biblia basi haiwalazimu wao kuwatendea haki, na wanadai kuwa hiyo ni hukumu ya Mwenyezi Mungu. Na wao wanajua vyema kuwa hayo ni kumzulia uwongo Mwenyezi Mungu. (Tazama katika Agano la Kale: Kumbukumbu la Torati, 23.19-20 inaruhusu kumnyonya riba mtu mbali asiyekuwa Yahudi. Kumbukumbu 12.21 inaruhusu kumlisha nyamafu mgeni na kumuuzia pia. Uzushi kama huu unakashifiwa na Aya 78 ifuatayo kuwa haya hayakutokana na Mwenyezi Mungu, bali wamepachika wao tu katika vitabu vyao.)
Hakika ni kweli wamemzulia uwongo Mwenyezi Mungu. Kwani mwenye kumrejeshea mwenyewe haki yake na akamtimizia kwa wakati wake kama alivyo ahidi, na akamwogopa Mwenyezi Mungu, wala asipunguze kitu wala asiakhirishe, huyo basi atapata mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwa sababu amemcha Yeye.
Wanao iacha ahadi ya Mwenyezi Mungu aliyo fungamana nao ya kuwa watazitimiza haki na watasimamia yaliyo waajibu, wala hawatoacha viapo vyao walivyo apa kuwa watatimiza - kwa thamani ndogo ya faida ya dunia, na ingawa kuu katika maoni yao, hao hawatakuwa na sehemu yoyote katika raha za Akhera. Mola wao Mlezi atawapuuza, wala hatowaangalia kwa jicho la rehema Siku ya Kiyama, wala hatowafutia dhambi zao, na watapata adhabu chungu ya kuendelea.