Mtindo wa wanaafiki ni kukungojeeni kama anavyo ngojea mwenye husda na maya anaye tamani mpate masaibu mnapo kuwa katika vita na maadui. Mkishinda kwa nusra ya Mwenyezi Mungu, na mkafungukiwa njia ya Haki, wao huwaambia Waumini - na hali wao ule ushindi walio pewa wenye Imani na Mwenyezi Mungu umewashtusha : Sisi hatukuwa nanyi? Kwa maana sisi ni jamaa zenu! Na ikiwa ni zamu ya makafiri kupata ushindi, basi wao huwaendea na kuwaambia: Sisi hatukuyashughulikia mambo yenu hata yakawa ni yetu? Na hatukukupeni mapenzi yetu, na tukakulindeni na hawa Waumini? (yaani sisi ni wenzenu). Na Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la atakuhukumuni baina yenu na hawa wanaafiki Siku ya Kiyama. Wala Mwenyezi Mungu hatowapa makafiri njia kuwashinda Waumini maadamu Waumini watashikamana na sifa ya Imani ya kweli na vitendo vyema.
Hakika wanaafiki, kwa ule unaafiki wao, wanadhani kuwa wanamkhadaa Mwenyezi Mungu Mtukufu na wanamficha hakika ya nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu Subhanahu ni Yeye ndiye anaye wakhadaa wao. Basi Yeye huwapururia kuwapa muhula, na anawawacha mpaka wabobee katika maovu yao, kisha ndio awahisabu kwa waliyo yatenda. Na hawa wanaafiki wana dhaahiri ya kuonekana, na ya ndani ya nafsi zao. Yale ya kuonekana ni vile kuwa wakiinuka kwenda kuswali huinuka kwa uvivu, kwa unyong'onyo. Na Swala yao ni riya tu, kuonyesha, si ya kweli. Na ya ndani ni kuwa hawakumbuki kumtaja Mwenyezi Mungu ila kwa nadra, kwa tukizi. Na lau kuwa wanamkumbuka vilivyo wangeli uacha unaafiki
Na hawa wanaafiki ni watu wanao taradadi, wanababaika. Kwenu hawapo, na kwao makafiri hawapo katika kila hali. Na hayo ni kwa sababu ya udhaifu wa imani, na udhaifu wa nafsi, na kwa sababu ya kupotoka na Haki. Na mwenye kuandikiwa kupotoka na Mwenyezi Mungu tangu hapo azali, basi huna njia wewe ya kumwongoa sawa.
Hakika katika sababu za unaafiki ni kuwa wanaafiki wamewafanya watu wasio kuwa Waumini kuwa ndio walinzi wao, marafiki zao, watawala wao, na ndio wa kuwanusuru. Enyi Waumini! Yaacheni haya, muepukane nayo. Wala msiwafanye makafiri ndio wa kukunusuruni, wakukutawalini, mkawanyenyekea. Na hapana shaka yoyote mkifanya hivyo mnampa Mwenyezi Mungu hoja iliyo wazi ya kukuhojini. Mtakuja ingia pamoja na wanaafiki, na mtadhalilika. Kwani inakuwa hamfanyi utukufu wenu utoke kwa Mwenyezi Mungu, na kwa haki, na vitendo vyema.
Hakika wanaafiki kwa sababu ya unaafiki wao watakuwa katika vina vya Jahannamu. Wao wako chini kabisa huko, na daraja ya mwisho kabisa. Wala hutompata wa kuwanusuru, wa kuwatetea na adhabu hiyo.
Isipo kuwa wale katika wao walio tubia, na wakarejea kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wakaungana naye Yeye peke yake, na wakajitakasa, na wakaelekeza nyuso zao kwake, na wakatenda mema. Wakifanya haya basi ndio wanakuwa miongoni mwa Waumini. Watapata malipo ya Waumini. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amekwisha waahidi Waumini malipo makubwa duniani na Akhera.
Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hana alitakalo kwenu ila mumuamini Yeye, na muishukuru neema yake. Mkiwa hivyo basi hampati adhabu, bali mtapata malipo ya kheri na shukrani. Kwani hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mwenye kushukuria waja wake kwa vitendo vyema, na ni Mjuzi, anajua hali zao zote njema na mbaya.