Je! Huijui hali ya wale walio pewa sehemu ya Kitabu na ilimu (nao ni Mayahudi na Wakristo) wanaitwa wende kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu, nacho ni Qur'ani ili kiwapambanulie baina ya Kweli na uwongo, Haki na baat'ili, katika khitilafu zilizo zuka baina yao, na wala hawafanyi haraka ya kumuitikia anaye waita. Bali baadhi yao wanamkataa; shani yao ni kuukataa wito wa kheri.
Hao wanao kataa miongoni mwa Mayahudi wamedanganyika kwa kukataa kwao na matumaini ya uwongo wanao jitamanisha nafsi zao ya kuwa Moto hautawagusa ila siku chache tu. Na kudanganyika huko na matamanio hayo yamewapelekea kuendelea kuzua katika dini yao kunako endelea.
Basi itakuwaje hali yao wakati atapo wakusanya Mwenyezi Mungu Siku ya Akhera, ambayo hapana shaka kuwapo kwake, na kuwa kutakuwapo kuhisabiwa. Basi kila nafsi itapewa malipo yake ya kutosha. Na wao wanastahili kupata hiyo adhabu ya Jahannamu watakayo ipata.
Ewe Nabii! Sema kwa unyenyekevu na kuukiri utukufu wake Mwenyezi Mungu: Ewe Mola Mlezi! Ni Wewe peke yako ndiye Mwenye kumiliki kutasarafu katika mambo yote. Unampa kuhukumu na utawala umtakaye, na unamnyima umtakaye. Unampa utukufu umpendaye kati ya waja wako kwa kumwezesha kuzishika sababu za kuufikia huo utukufu. Na unampiga madhila na unyonge umtakaye. Basi Wewe peke yako unamiliki kheri yote. Hushindwi na kitu katika kutimiza muradi wako na yanayo kupelekea hikima yako kuyakatia shauri katika mipango ya uumbaji wako.
Na Wewe kwa ulivyo umba na ukawekea sababu na nyendo, unauingiza usiku katika mchana kwa unavyo zidi mchana urefu wake, na unauingiza mchana katika usiku kwa unavyo zidi usiku urefu wake. Na unatoa chenye sifa za kuonekana kihai katika kisicho kuwa na sifa za uhai, kama unavyo toa chenye kukosa uhai kutokana na kilicho hai, chenye kutamakani na sababu za uhai. Unampa neema zako kubwa umtakaye kwa mujibu wa mipango ya hikima zako. Hapana mchunguzi wa kukuhisabu Wewe. Huyo Mwenye shani hii haemewi na kumjaalia Mtume wake na awapendao, ubwana, na utawala, na utajiri, na wasaa, kama alivyo waahidi.
Ikiwa basi ni Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taa'la ndiye Yeye peke yake Mmiliki wa mamlaka, anatukuza na kuangusha, na katika mikono yake pekee ipo kheri, na uumbaji, na riziki, basi haifai kwa Waumini kuwafanya wasio kuwa Waumini wawe na utawala juu yao, wakauwacha msaada wa Waumini wenzao. Kwani wakifanya haya inakuwa wanaivunja Dini, na wanawaletea maudhi wenye Dini, na ni kuudhoofisha utawala na udugu wa Kiislamu. Na mwenye kufuata njia hii basi kwa Mwenyezi Mungu Mmiliki wa mamlaka yote hana lake jambo. Wala haimfalii Muumini kuridhia kuwapa utawala na ulinzi makafiri ila awe hana hila. Hapo basi anaweza kujikinga na madhara yao kwa kuonyesha ut'iifu kwao. Ni juu ya Waumini wawe daima katika ulinzi wa Kiislamu, kwani huo ndio ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Na watahadhari wasitoke kwenye ulinzi wa Mwenyezi Mungu kuuendea ulinzi mwenginewe asije akawaadhibu kwa kuwaletea madhila baada ya utukufu. Na kwake Yeye ndio marejeo, wala hapana pa kukimbilia kutokana na madaraka yake duniani wala Akhera.
Sema, ewe Nabii!: Mkiyaficha yaliyomo vifuani mwenu au mkiyadhihirisha katika vitendo vyenu na kauli zenu ni sawa, kwani Mwenyezi Mungu anayajua yote, na anayajua yote yaliymo mbinguni na yaliyomo duniani, yanayo onekana na yanayo fichikana. Uwezo wake unapenya katika viumbe vyake vyote.