Harufi hizi na mfano wa hizi ndizo zikakusanyika kuifanya Qur'ani kuwa ni muujiza ulio washinda watu kuiga mfano wake, ijapo kuwa hizo harufi ndizo wanazo zitamka. Basi mwenye kuitilia shaka hii Qur'ani kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu au la, basi na alete mfano wake. Na hatoweza.
Sisi tunaweza kuwaletea muujiza wa kuwalazimisha Imani, wat'ii kwa unyenyekevu amri yake, na yatimie unayo yatarajia. Lakini hatuwaletei, kwa sababu mwendo wetu ni kuwaongoza watu waamini bila ya kuwalazimisha, ili isikosekane hikima ya kujaribiwa kwa mitihani, na yanayo kuja baada yake ya thawabu na adhabu.
Wala Mwenyezi Mungu hawaletei watu wako kwa ufunuo wake ya kuwakumbusha Dini ya Haki kuwa ni rehema kwao, ila wao huzua upya upinzani na ukafiri kuukataa. Kwani njia ya uwongofu imekwisha zibwa mbele yao.
Hawa hakika wamekadhibisha Haki uliyo ileta, na wakaifanyia maskhara. Lakini wewe wasubirie. Wataona matokeo ya maskhara yao ya kuangamiza.
Hivyo hao wanatenda watendavyo katika ukafiri wao na kukadhibisha kwao wala hawaangalii baadhi ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu katika hii hii ardhi? Lau kuwa wanaangalia kwa kuzingatia wangeli ongoka. Hebu wazingatie hii mimea ya kila namna yenye manufaa tunayo itoa Sisi kwenye ardhi, na wala hawezi hayo isipo kuwa Mungu Mmoja Muweza.
Ewe Muhammad! Watajie watu wako kisa cha Musa pale Mola wako Mlezi alipo mwita: Ewe Musa! Nenda kwa Utume kwa watu walio dhulumu nafsi zao kwa ukafiri, na wakawadhulumu Wana wa Israili kwa kuwafanya watumwa na kuwauwa watoto wao wanaume.
Na mimi nimejaa dhiki kwa kuwa wataniambia mwongo, na ulimi wangu si mkunjufu wa kuweza kuhojiana nao kama ninavyo penda. Basi mtume Jibril ende kwa ndugu yangu aje kuniunga mkono katika hii kazi yangu.
Na watu hawa wana kisasi juu yangu. Kwani mimi nilimuuwa mtu katika wao. Basi nina khofu watakuja niuwa kwa kisasi kabla sijatimiza kazi yangu. Hayo yananizidisha khofu.
Mwenyezi Mungu akamwambia: Hawatokuuwa. Na kwa mintarafu ya Haruni nimekukubalia ombi lako. Basi nendeni nanyi mmejizatiti na miujiza yetu. Mimi niko pamoja nanyi kwa ulinzi. Nayasikia yanayo jiri baina yenu na Firauni. Nyinyi mtapata ushindi, na kuungwa mkono.
Firauni akamwambia Musa kwa kumsimbulia, naye alimtambua walipo ingia na wakakadimisha Ujumbe wao, kwani alilelewa mle mle katika kasri lake: Hatukukulea sisi ulipo kuwa mtoto? Na ukaishi chini ya ulezi wetu kwa miaka mingi katika umri wako?
Na ukatenda makosa yako ya jinaya maovu kumuuwa mtu katika kaumu yangu, na ukazikanusha neema zangu nilizo kufanyia, hukuwahifadhi raia zangu, ukaushambulia ungu wetu kwa kudai kuwa wewe ati ni Mtume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.