Mwenyezi Mungu amewaruhusu Waumini wanao pigwa vita na washirikina wawarejezee uadui wao, kwa sababu ya dhulma iliyo wapata nao wakasubiri kwa muda mrefu. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuweza kuwanusuru vipenzi vyake Waumini. " Wameruhusiwa kupigana wale wanao pigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia" Yaliyo tajwa na Qur'ani Tukufu kukhusu hukumu iliomo katika Aya 39 yamezitangulia kanuni zilizo kuja kuwekwa na madola baada yake, nayo ni kuwa mtu kujitetea nafsi yake ni sharia vyovyote vile itavyo kuwa matokeo yake. Na kwamba mwenye kuitetea nafsi yake, na mali yake, na nchi yake, hawi ni mkosa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya uadilifu, ijapo kuwa ameuwa mtu au ameteketeza roho nyingi. Aya hii imepasisha kuwa Waislamu wanayo ruhusa kujitetea pindi wakivamiwa. Na kwa hivyo tunafahamu kuwa vita vya Waislamu vilikuwa vita vya utetezi na kujilinda si vita vya kushambulia na kuvamia. Na kwamba Waislamu waliusimamisha Uislamu na wakaupa nguvu kwa hoja zilizo wazi, na dalili zilizo dhaahiri.
Hao ambao makafiri wamewadhulumu na wakawalazimisha waache mji wao wa Makka wauhame. Na wao hawakuwa na kosa lolote ila ni kuwa walimjua Mwenyezi Mungu na wakamuabudu Yeye pekee. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwatumilia kwa ajili ya Haki wasaidizi wa kumnusuru Yeye na wakamtetea kupinga jeuri za madhaalimu, basi hapana shaka upotovu ungeli enea, na majeuri wangeli endelea katika jeuri zao, na sauti ya haki wangeli inyamazisha. Wala wasingeli achiliwa Wakristo makanisa yao, wala mamonaki (wat'awa wa Kikristo) wasinge baki na monastari zao (nyumba zao za ibada), wala Mayahudi wansinge kuwa na masinagogi yao, wala Waislamu wasinge kuwa na misikiti yao, ambamo mote humo hutajwa kwa wingi jina la Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu amechukua juu ya nafsi yake ahadi ya nguvu ya kwamba atamsaidia na kumnusuru kila anaye isaidia Dini yake, na atamtukuza kila mwenye kulitukuza Neno la Haki katika ulimwengu. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu haiendi kinyume. Kwani Yeye ni Mwenye nguvu wa kutimiza alitakalo, Mtukufu hashindwi na yeyote.
Hao Waumini tulio waahidi kuwanusuru ndio hao ambao tukiwapa madaraka katika nchi wanalinda makhusiano yao na Mwenyezi Mungu na pia na wanaadamu wenzao. Kwa hivyo hushika Swala kwa utimilifu wake, na huwapa Zaka wanao stahiki kupewa, na huamrisha kila lenye kheri, na hukataza kila lenye shari. Na mambo yote hurejea kwa Mwenyezi Mungu peke yake. Basi Yeye humtukuza amtakaye, na humdhalilisha amtakaye.
Ewe Nabii! Ukiwa unapata makanusho, kuambiwa mwongo, na maudhi kutokana na watu wako, basi usisikitike. Zingatia taarikh kwa yaliyo wapata Mitume wa kabla yako, utaona kwamba wewe si Mtume wa kwanza aliye kanushwa na kuudhiwa na watu wake. Kwani kabla ya hawa walio kukanusha wewe, kaumu Nuhu walimkadhibisha Mtume wao Nuhu, na kaumu ya A'ad walimkadhibisha Mtume wao Huud, na kina Thamud walimkanusha Mtume wao Swaleh.
Na watu wa Madiana walimkanusha Mtume wao Shua'ib. Na Firauni na watu wake walimkanusha Mtume wa Mwenyezi Mungu Musa. Mitume hao wote yaliwapata yanayo kupata wewe. Na Mimi niliwapa muhula hao wakanushao ili wapate kutubia waongoke, na waitikie Wito wa Haki. Lakini wakazua na wakaendelea na kuwakadhibisha Mitume wao na kuwaudhi. Wakazidisha madhambi juu ya madhambi yao. Basi nikawaadhibu ukomo wa kuwaadhibu. Angalia taarikhi yao utaona kuwa adhabu yangu ilikuwa kali mno, pale nilipo ibadilisha neema ikawa nakama, na uzima ukawa ni maangamizo, na badala ya ujenzi ukawa uharibifu.
Basi tuliwatekeza watu wengi wa miji ambayo waliiamirisha, kwa sababu ya udhalimu wao na kukanusha kwao Mitume wao. Zikawa paa za nyumba zao zimeangukia kuta zake, hazina wakaazi. Kama kwamba jana hazikuwapo. Visima vingapi vilivyo bomoka na maji yake yakapotea, na majumba mangapi madhubuti yaliyo jengwa kwa mawe na saruji na chokaa, yamekuwa magofu hayana wakaazi!
Hivyo wao wanasema wayasemayo na wanahimiza waletewe adhabu, nao hawatembei ulimwenguni wakaona kwa macho yao walivyo teketea hao madhaalimu wakanushao? Huenda hapo nyoyo zao zikagutuka kutokana na ghafla iliyo wapamba, na wakatia akilini yanao wapasa wakafuata hayo ya wito wa Haki unao waitia. Na masikio yao yakisikia vifo vya hao makafiri huenda wao wakazingatia. Lakini wapi! Ya mbali hayo kuwa watu hawa waweze kuzingatia kwa wanayo yaona au kuyasikia maadamu nyoyo zao zimekuwa kama mawe. Kwani kipofu wa kweli siye yule aliye pofuka macho, lakini ni yule aliye pofuka moyo na hatambui kitu.