Mwenyezi Mungu hakumchukua yeyote kuwa ni mwanawe. Yeye ametakasikia na hayo. Wala hana mshirika. Angeli kuwa na mshirika basi kila mmoja wao angejipa madaraka ya pekee kwa alivyo viumba, na vikawa ndio milki yake, na wangeli gombana wenyewe kwa wenyewe kama wanavyo onekana wafalme wanavyo fanya. Na ulimwengu ungeli fisidika kwa mizozano hiyo. Basi Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wayasemayo washirikina yanayo kwenda kinyume na Haki.
Na Yeye amevizunguka vitu vyote kwa kuvijua. Anajua tusiyo yaona na tunayo yaona. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mnasibisha nayo makafiri kuwa ati ana washirika.
Wewe endelea na wito wako, na ukabili uovu wao kwa vitendo vilivyo vizuri kama kusamehe au vyenginevyo. Na Sisi tunajua vyema wanakutaja vipi wewe, na wanavyo usema kwa ubaya huo wito wako kwa uwovu na uzushi. Na Sisi tutawalipa kwa hayo.
Ili nipate kufanya a'mali njema katika mali au wakati nilio acha. Wala ombi lake halitokubaliwa. Kwani haya ni maneno anayasema bila ya faida, hayakubaliwi. Na pindi akikubaliwa hatotenda kitu. Na juu ya yote hatorudi kabisa! Kwani mauti ni kizuizi baina yao na hayo wanayo yatamani mpaka Mwenyezi Mungu atapo wafufua.
Ukifika wakati wa kufufuliwa tutawafufua kutoka makaburini kwao. Na hayo ni kwa mfano wa kupulizwa tarumbeta watafufuka nao wamefarikiana. Hapana mtu utaomfaa ujamaa wake na fulani. (Ujamaa Kiswahili maana yake makhusiano ya nasaba, sio usoshalisti.) Wala hapana mtu atae muomba mtu kitu cha kumfaa. Kwani kila mmoja wao siku hiyo atakuwa kashughulika na lake.
Na asiye kuwa na thawabu au vitendo vyenye uzito mbele ya Mwenyezi Mungu, hao ndio walio zikhasiri nafsi zao kwa kuziuza kwa Shetani. Nao wataadhibiwa Motoni, wadumu humo.