Uingieni, mpate kuonja vukuto lake. Mkivumilia shida zake, au mkitovumilia, kwenu ni mamoja. Hakika leo mtayakuta mliyo kuwa mkiyatenda duniani.
Na walio amini, na wakastahiki vyeo vya juu, na vizazi vyao wakawafuata katika Imani, na wao hawajafikia daraja zile za baba zao, tutawakutanisha nao hao dhuriya zao, wapate kutulia nyoyo zao. Na wala hatuwapunguzii chochote katika thawabu za vitendo vyao. Wala wazazi hawatobeba chembe katika makosa ya dhuriya zao. Kwa sababu kila mtu amefungamana kwa rahani na vitendo vyake visio bebwa na mwenginewe.
Huko Peponi watakuwa wakipeana kwa mapenzi bilauri zilio jaa vinywaji visio leta maneno yasiyo na maana wala vitendo vya dhambi, yaani havilevi na kuondoa akili.
Wewe endelea na kukumbusha kama unavyo fanya. Kwani wewe, kwa neema ya Mwenyezi Mungu aliyo kuneemesha kukupa Unabii na akili iliyo timia, si kuhani anaye toa khabari za ghaibu bila ya ilimu, wala si mwendawazimu unaye sema usiyo yasadiki.
Bali ndio akili zao zinawaamrisha waseme maneno hayo yanayo gongana. Kwani kohani na mtunga mashairi ni watu wenye fahamu na akili; na mwendawazimu hana akili. Lakini hawa ni watu walio pita mipaka katika inadi zao.
Kwani wao ndio walio ziumba mbingu na ardhi kwa uumbaji mzuri wa pekee wa namna hii? Bali wao hawana na yakini na lolote lilio mwajibikia Muumbaji. Na kwa hivyo ndio wanamshirikisha.
Bali wanacho kipandio cha kupandia mpaka mbinguni wakasikiliza anayo yahukumia Mwenyezi Mungu? Kama hivyo, basi nawamlete huyo mtu wao anaye sikiliza atoe hoja iliyo wazi kuthibitisha madai yake.
Au wao wanae mungu wa kuabudiwa badala ya Mwenyezi Mungu atakae walinda na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ametakasika na hayo wanayo mshirikisha naye!
Na hakika hao walio dhulumu watapata adhabu mbali na hii waliyo teseka nayo hapa duniani, lakini wengi wao hawajui hayo.
Wewe isubirie hukumu ya Mola wako Mlezi ya kuwapa muhula hao, na wewe kupata maudhi yao. Kwani hakika wewe umo katika hifadhi yetu na ulinzi wetu. Basi vitimbi vyao havitokudhuru wewe. Na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo amka.