Na mwanamume aliye iba, na mwanamke aliye iba, ikateni mikono yao kuwa ni malipo ya madhambi waliyo yatenda, na njia ya kuwaonya wenginewe wasitende jambo hilo. Hiyo ni hukumu ya Mwenyezi Mungu, na amri ya Mwenyezi Mungu ndiyo yenye kushinda, naye ndiye Mwenye hikima katika kutunga Sharia. Kila ukhalifu ameuwekea malipo yake, yenye kumzuia mtu asitende tena na wengine watahadhari wasifanye kama hayo. (Ajabu iliopo ni kuwepo wajinga wakashtushwa na amri hii ya Mwenyezi Mungu aliye tuumba, na wasiseme lolote kuwa katika China wakati wa vita na Taiwan ilikuwapo sharia ya kuwa mwizi auwawe, na katika baadhi ya wilaya za Amerika mpaka hii leo ipo sharia ya kuwa mwizi wa farasi auwawe, na katika Kenya adabu ya wizi wa kutumia nguvu ni kunyongwa, na katika sharia za Kiingereza na nchi zote za magharibi mtu ana haki ya kuuwa kwa ajili ya kulinda mali na roho. Ikiwa ni haki ya mtu kumuuwa atakaye kuja kwiba, jee ni kuu hilo kwa serikali kumkata mkono aliye kwisha iba?) Kwa kuwepo sharia kama hii ndiyo ikawa wizi umetoweka katika nchi kama Saudi Arabia, na ukawa vururu kwengineko.
Lakini mwenye kutubu baada ya kutenda kosa lake hilo, na akatengeneza vitendo vyake, na akanyoosha mwendo wake, basi Mwenyezi Mungu hakika humkubalia toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi mno wa kusamehe na kurehemu.
Jua, ewe mwenye fahamu, kwa ujuzi wa yakini, ya kwamba ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye kumiliki kila kitu kiliomo katika mbingu na ardhi. Yeye humpa adhabu yake amtakaye, kwa hikima yake na uwezo wake. Na humsamehe amtakaye, kwa hikima yake na rehema yake. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Ewe Mtume! Visikuhuzunishe vitendo vya makafiri wanao wania ukafiri wa kila aina, hawa wadanganyifu wenye khadaa wasemao kwa ndimi zao: Tumeamini, ilhali nyoyo zao hazifuati haki. Na miongoni mwa Mayahudi wapo wanao kithiri kusikiliza uzushi wa makohani wao na wanayakubali, na wanakisikiliza na kukikubali kikundi maalumu miongoni mwao, na hawaji barazani kwako kwa sababu ya kiburi na chuki! Na hawa huyageuza maneno ya Taurati kutokana pahala pake, baada ya Mwenyezi Mungu kwisha yasimamisha na kuyahukumia! Nao huwaambia wafwasi wao: Mkipewa maneno haya yaliyo potoshwa na kubadilishwa yakubalini na muyafuate. Na kama mkipewa mengine tahadharini nayo msiyakubali. Basi, ewe Mtume! Usihuzunike Mwenyezi Mungu akimhukumia mtu kupotea kwa kumziba moyo wake, wewe hutoweza kumwongoa, au kumnafiisha kwa chochote asicho mtakia Mwenyezi Mungu. Na hao ndio walio pita mipaka katika upotovu na inda. Mwenyezi Mungu Mwenyewe hakutaka kuzisafisha nyoyo zao na uchafu wa chuki, na inadi, na ukafiri. Duniani watapata madhila, kwa kufedheheka na kushindwa, na Akhera watapata adhabu kuu.