Na Mayahudi na Wakristo husema: Sisi ndio tulio fadhiliwa, kwani sisi ndio wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake atupendao. Waambie ewe Mtume! Basi kwa nini anakuadhibuni kwa dhambi zenu, na anakutieni katika moto wa Jahannamu? Waongo nyinyi! Nyinyi, kama wanaadamu wengineo, ni viumbe, na mtahisabiwa kwa vitendo vyenu. Na maghfira yamo mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake, humsamehe amtakaye. Na adhabu yake ni kwa amtakaye kumuadhibu. Kwani ufalme wa mbingu na ardhi na viliomo baina yao ni wa Mwenyezi Mungu tu, na kwake Yeye ndio marejeo ya mwisho.
Enyi Watu wa Kitabu! Umekujieni ujumbe wa Mtume wetu ambaye anakudhihirishieni Haki, baada ya kusita ujumbe kwa muda wa zama, ili msitafute udhuru wa ukafiri wenu, kwa kudai ati kuwa Mwenyezi Mungu hakukuleteeni mbashiri wa kukupeni khabari njema, wala mwonyaji wa kukuhadharisheni. Sasa, basi, huyo amekujilieni mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila jambo - na katika hayo mambo ni kutuma Mitume, na kukuhisabuni kwa mliyo nayo.
Na taja, ewe Mtume! pale Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu kwa kushukuru na kut'ii, kwa kuwa amewateua Manabii wengi miongoni mwenu, na akakufanyeni watukufu kama wafalme baada ya kuwa mlikuwa wanyonge chini ya utawala wa Firauni, na akakupeni neema nyingi nyenginezo ambazo hawajapewa wowote wengineo.
Enyi watu wangu! T'iini amri ya Mwenyezi Mungu. Ingieni ardhi takatifu aliyo kujaalieni Mwenyezi Mungu muingie, wala msirejee nyuma kuwaogopa hao watu wake majabari, mkaja kukosa nusura ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.
Wana wa Israili wakaikhalifu amri ya Mwenyezi Mungu na wakasema: Ewe Musa! Katika nchi hii wamo watu majabari. Sisi hatuna nguvu za kupambana nao. Basi hatutoingia humo maadamu wao wamo. Wakitoka basi tena hapo sisi tutaingia.
Wawili kati ya wakubwa wao walio kuwa wanamwogopa Mwenyezi Mungu, na ambao Mwenyezi Mungu amewapa neema ya imani na ut'iifu, walisema: Enyi watu! Waingilieni hao majabari wa mjini kwa kupitia mlangoni kwa ghafla. Mkifanya hivyo nyinyi mtawashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu peke yake katika mambo yenu yote, ikiwa nyiny ni wenye Imani ya kweli.