Wajumbe walifika kwa Sayyidina Sulaiman na zawadi zao. Huku anazijua neema za Mwenyezi Mungu Mtukufu zilio juu yake, Akawaambia naye ndio anamsemeza huyo Malkia na watu wake katika mkabala na wajumbe: Hivyo ndio mnanipa mimi mali? Aliyo nipa Mwenyezi Mungu ya Unabii, na ufalme, na neema, ni makubwa zaidi kuliko aliyo kupeni nyinyi. Bali nyinyi kwa hizi zawadi zenu na wingi wa mali yenu mnafurahi, sio kama mimi. Kwa sababu nyinyi hamjui ila yaliyo shikamana na dunia hii tu.
Akasema, akimsemeza yule msemaji kwa jina lao: Ewe mjumbe! Rejea kwao. Wallahi! tutawatokea kwa majeshi wasio yaweza kupambana nayo na kuyakabili. Na tutawatoa kwenye nchi ya Sabai nao wamepoteza utukufu wao, wamefanywa watumwa.
Sulaiman akawaelekea binaadamu na majini aliyo dhalilishiwa na Mwenyezi Mungu kumtumikia, akawashitua kwa jambo geni. Akasema: Ni nani katika nyinyi anaweza kuniletea kiti chake cha enzi kikubwa kabla hawajanijia nao wamekwisha nyenyekea wanat'ii.
Mmoja pandikizi la kijini lilisema: Mimi nitakuletea, na wewe umekaa katika baraza yako hii, kabla hujaondoka. Na mimi hakika naweza hayo, na muaminifu katika maneno yangu na vitendo vyangu.
Akasema aliye pewa nguvu za kiroho, na ilimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea hicho kiti cha enzi kabla jicho lako halijapepesa. Na akatimiza aliyo yasema. Sulaiman alipo kiona kiti kile kimetua mbele yake bila ya mtingisiko, alisema: Haya ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu aliye niumba na akanipa kheri zake ili anifanyie mtihani, nitashukuru kwa neema hizi au sitoi haki yake? Na mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu basi huyo hakika amejiondolea nafsi yake mzigo wa waajibu. Na mwenye kuacha kushukuru kwa neema basi hakika Mola wangu Mlezi ni Mkwasi, si mwenye kuhitajia shukrani. Naye ni Karimu wa kuneemesha.
Sulaiman akawaambia watu wake: Kigeuzeni geuzeni hichi kiti cha enzi kwa baadhi ya mabadiliko ya nje, tupate kuona atakijua kwa kukiendea au hato kijua na kwa hivyo hato kiendea.
Alipo fika jicho lake lilipiga kwenye kiti chake cha enzi. Akaambiwa: Je! Kiti chako cha enzi ni mfano wa hiki? Akasema kwa vile kilivyo kamilika kufanana: Kama kwamba ndicho hichi. Na Sulaiman na walio pamoja naye wakasema: Sisi tulisha pewa ujuzi kumjua Mwenyezi Mungu na uwezo wake na ukweli wa yaliyo kuja kutoka kwake kama anavyo jua mwanamke huyu. Na sisi tangu hapo ni watu tulio mfuata Mwenyezi Mungu na tunamsafia Yeye ibada.
Na zile ibada za jua na mfano wake zilimzuia yule Malkia kumuabudu Mwenyezi Mungu. Kwani yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.
Baada ya hao akaambiwa: Ingia katika jumba la Sulaiman. Na uwanja wake wa ndani ulikuwa umesakafiwa kwa kiyoo, na chini yake maji, na samaki wakiogelea humo. Kupandisha nguo miundi yake ya miguu ikaonekana, kwa kuwa alidhania ni maji. Sulaiman akamwambia hicho ni kiyoo, basi yakamuathiri yale madhaahiri ya kilimwengu, na akaona kuwa ufalme wake yeye haufai chochote mbele ya ufalme wa Nabii Sulaiman. Akasema: Mola Mlezi! Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu kwa kughurika na ufalme wangu na ukafiri wangu. Na sasa ninanyenyekea pamoja na Sulaiman kumuamini Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye kuumba walimwengu wote na kuwalea na kuwasimamia.