T'aa Siin, (T' na S) harufi mbili za kutamkwa, ni harufi za alifbete, ndizo zimeanzia Sura hii, ili kunabihisha siri ya muujiza wa Qur'ani pamoja na kuashiria kuwa imeundwa kwa jinsi ya harufi hizi hizi mnazo zitumia katika kusema, na pia kuzindua akili ziisikilize hii Qur'ani inapo somwa. Hizi Aya zilizo teremka kwa kusomwa, na ni Kitabu chenye kubainisha mambo yaliyo kuja ndani yake.
Waumini hao ndio wanao ishika Swala kwa unyenyekevu na kutimiliza nguzo, na wanatoa Zaka kwa nyakati zake, nao wana yakini ya maisha ya baadaye Akhera, na yatayo kuwa huko ya adhabu na thawabu.
Hakika wale ambao hawaiamini Akhera, Sisi tumewapambia vitendo vyao kwa kuwaumbia matamanio ndani yake. Kwa hivyo wao wanababaika humo katika upotovu wao.
Ewe Nabii! Wewe unapokea Qur'ani hii unayo teremshiwa kutokana na Yeye ambaye hapana anaye mkaribia kwa hikima yake, naye anajua kila kitu.
Kumbuka pale Musa alipo mwambia mkewe na walio pamoja naye na yeye ndio anarejea Misri: Mimi nimeona moto. Nitakwenda kuleteeni khabari ya njia, au nitapata kijinga cha moto, kitacho kufaeni kwa kuota moto kwa hii baridi.
Alipo fika huko paliitwa: Wamebarikiwa waliomo katika moto huu na walioko pembezoni mwake, yaani karibu yake. Nao ni Malaika na Musa. Na Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote ametakasika na kila kisicho kuwa laiki naye.
Na katika njia ya kufikisha wito wako, tupa fimbo yako na utaiona inatikisika kama kijoka jepesi kinakwenda mbio. Yeye akarudi nyuma, wala hakurejea baada ya kurudi nyuma. Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtuza kwa kauli yake: Usiogope. Mbele yangu hawaogopi. Mitume ninapo sema nao. Kisa cha Musa kimetajwa zaidi ya mara moja katika Qur'ani. Pengine hutolewa yasiyo tajwa penginepo. Na kila sehemu ina mnasaba wake. Katika sehemu hii makusudio ni kuondoa yale mastaajabu ya kuwa Nabii Muhammad s.a.w. kapata Ufunuoa (Wahyi) vile vile.
Lakini mwenye kutenda asicho ruhusiwa, na kisha akaleta wema baada ya kuteleza kwake, basi Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mkubwa wa kurehemu.
Na utie mkono wako katika mfuko wa nguo zako, utatoka mweupe wala si kwa balanga. Hayo ni katika Ishara tisa za kumpelekea Firauni na kaumu yake. Hakika hao walikuwa watu walio tokana na amri ya Mwenyezi Mungu, ni makafiri. Hizo Ishara tisa ni:- Kupasuka bahari, T'ufani (Kimbunga), Nzige, Chawa, Vyura, Damu, Ukame, Fimbo, Kutoka mkono mweupe bila ya maradhi.