Na enyi watu! Hizi khitilafu ziliopo baina yangu na nyinyi zisikupelekeeni kufanya inda na mkashikilia ukafiri, hata yakakupateni yaliyo wapata kaumu ya Nuhu, na kaumu ya Huud, na kaumu ya Swaleh. Na wala zama na pahala pa kaumu Lut' na maangamizo yao si mbali nanyi! Basi zingatieni yasikusibuni yaliyo wasibu hao.
Na mtakeni Mwenyezi Mungu akusameheni madhambi yenu, na rejeeni kwake kwa majuto mkiomba maghfira kila mtendapo dhambi. Hakika Mola wangu Mlezi ni mwingi wa rehema, ni mwenye mapenzi. Huwasamehe wenye kutubu, na anawapenda wenye kurejea kwake.
Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi unayo yasema sisi hatuyafahamu! Na sisi tunakuhakikishia kuwa sisi tunakuona wewe dhaifu, huna nguvu zozote za kujitetea, wala kutukinaisha tukitaka kukutenda unayo yachukia. Na lau kuwa si kwa wema wetu kwa jamaa zako, kwani wao wanafuata dini yetu, tungeli kuulia mbali kwa kukupiga mawe. Na wewe si mtukufu kati yetu hata tukutukuze, na tukuhishimu, na tukukirimu na tuache kukuuwa kwa mawe! Ni wema tunao wafanyia jamaa zako tu ndio unao tuzuia tusikuuwe.
Akasema Shua'ibu: Enyi watu wangu! Hivyo jamaa zangu ndio wanastahiki kufanyiwa wema kuliko Mwenyezi Mungu. Wao mnawakumbuka, na mkataka kunifanyia jamala mimi kwa ajili yao. Lakini Yeye mmemsahau na mkamfanya kama kitu kilicho tupiliwa mbali nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola Mlezi wangu ni Mwenye kuyazunguka yote mnayo yafanya kwa kuyajua, hapana linalo fichikana kwake katika vitendo vyenu, na atakuhisabieni kwavyo hata ikiwa nyinyi mtasahau.
Enyi watu wangu! Tendeni mnayo weza nyinyi kuyatenda. Kama hamsikilizi nasaha zangu, mimi naendelea kushikilia kutenda kinyume na vitendo vyenu. Na hapo tutakuja jua ni nani kati yetu ataye fikiwa na adhabu ya kumfedhehi na kumdhalilisha, na ni nani kati yetu ni mwongo - mimi ninaye kuonyeni na adhabu, au nyinyi mnao nionya kunifukuza katika mji wenu? Ngojeeni nini litatokea, na mimi nangojea pamoja nanyi.
Ilipo kuja amri yetu ya kuwaadhibu na kuwaangamiza, tulimwokoa Shua'ibu na walio amini pamoja naye wasipate adhabu na maangamizo. Kuokoka kwao kulikuwa kutokana na rehema iliyo tokana nasi. Ukelele uliwatwaa watu wa Madyana, na tetemeko la kuteketeza, wakapambaukiwa wamekwisha jifia katika majumba yao, wamelala kifudifudi, hawatukusiki hata kidogo!
Mambo yakawishia, na athari zao zikapotea. Wakawa kama kwamba hawajapata kukaa katika majumba yao! Hali yao ikatamka ya kumzindua kila mwenye akili apate kuzingatia! Zingatia basi maangamizo ya Madyana, na vipi walivyo baidika na rehema ya Mwenyezi Mungu kama walivyo baidika watu wa Thamud kabla yao!
Tulimtuma ende kwa Firauni na wakuu katika watu wake. Firauni akamkanya Musa na akawaamrisha watu wake wamfuate yeye Firauni katika ukafiri wake. Wakenda kinyume na amri ya Musa! Wala amri ya Firauni haikuwa ni nyoofu yenye matokea mema hata istahiki kufuatwa.