Wauweni walio kuanzeni vita popote mnapowakuta, na watoeni Makka, wat'ani wenu ambao wamekulazimisheni kuutoka. Wala msione vibaya, kwani walio kufanyieni nyinyi ni maovu zaidi kuliko kuuwa msikitini, nako ni kuwafitini Waumini katika Dini yao kwa kuwaadhibu huko Makka mpaka wakauacha mji wao kuhifadhi Dini yao. Na huu Msikiti Mtakatifu una utakatifu wake, basi msiuvunje kwa kupigana ndani yake. Lakini wakikupigeni vita ndani yake basi nanyi pia wauweni, na nyinyi kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu, mtashinda. Na malipo ya makafiri ni kufanyiwa wanayo wafanyia watu.
Wakirejea wakaacha ukafiri, wakafuata Uislamu basi Uislamu humuitikia anaye uelekea. Na Mwenyezi Mungu atawasamehe ule ukafiri wao wa zamani kwa fadhila yake na rehema yake.
Wapigeni vita walio taka kukuuweni na kukugeuzeni muache Dini yenu kwa maudhi na mateso mpaka ing'oke mizizi ya fitina na isafike Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Wakiuacha ukafiri wao basi wamejiokoa nafsi zao na wataepukana na adhabu. Hapo basi haifai kuwafanyia uadui. Uadui hufanyiwa mwenye kuidhulumu nafsi yake akaiteketeza kwa maasi na akaacha uadilifu kwa maneno na vitendo.
Na pindi wakikushambulieni katika mwezi mtukufu msiache kupigana nao, kwani huo ni mtukufu kwao kama ulivyo kuwa mtukufu kwenu. Ikiwa wao watauvunja utukufu wake basi nanyi wakabilini kwa kuzilinda nafsi zenu katika huo mwezi. Na katika mambo matukufu na matakatifu pana sharia ya kisasi na kutendeana mfano kwa mfano. Anaye kushambulieni katika matakatifu yenu nanyi jilindeni na uadui huo kwa mfano wake. Na mcheni Mwenyezi Mungu, msikiuke mipaka katika kulipiza kisasi. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwanusuru wachamngu.
Kupambana na makafiri kunahitaji kutoa roho kama ilivyo kutoa mali. Basi toeni kwa kuandaa vita, na jueni kuwa kupigana na hawa ni kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi msikae tu. Toeni mali kwa ajili yake, kwani mkitofanya na mkafanya ubakhili adui atakupandeni na atakudhilini. Hapo itakuwa kama mlio jitokomeza wenyewe kwenye maangamio. Tendeni lilio kuwajibikieni kwa uzuri na vilivyo, kwani Mwenyezi Mungu hupenda anapo fanya jambo mtu alifanye vizuri. Aya 190 mpaka 195 zinaeleza sharia ya vita katika Uislamu. Nazo zinaeleza kwa matamshi yalio wazi haya yafuatayo: 1. Ruhusa ya kupigana imetolewa kwa ajili ya kujilinda na uvamizi wa vita wa vitendo khasa, au zikidhihiri dalili kuwa maadui wanataka vita. Vita havikulazimishwa kwa ajili ya vita wala kwa sababu ya kutaka kuwasilimisha watu kwa kuwauwa na kuwapiga vita. 2. Kunakatazwa kuvamia au kuanza uadui kwa njia yoyote ile. Basi hapana ruhusa kufanyiwa uadui asiye pigana, wala hapana ruhusa kuvuka mipaka ya uadui wakati wa vita: basi hauliwi asiye chukua silaha, wala hakhusiani na vita bali ni mwenye kukumbwa tu na vita. Wala hauliwi mwenye kusalimu amri na akatupa silaha. Wala hapana ruhusa kuwavunjia watu nyumba zao, huko ni kupita mpaka. 3. Mzingatie fadhila iliyo onyeshwa kwa kuamrishwa kuchamngu. Basi msivunje heshima ya wanawake kuwanajisi, hata washirikina wakifanya hayo. Wala msiwakatekate walio uwawa hata ikiwa makafiri wakiwafanyia hayo Waumini. Washirikina walimfanyia hayo Bwana wa Mashahidi, Hamza, wala Mtume s.a.w. hakutoa ruhusa kumfanyia hayo maiti yeyote, bali alikataza akasema:"Tahadharini msiwakatekate maiti". 4. Vita vinakwisha wakiacha washirikina kuwafitini Waumini katika Dini yao, na Dini inakuwa inataka akili na nyoyo zimwelekee Mwenyezi Mungu kwa uhuru. 5. Hapana vita katika mwezi mtukufu, nayo ni miezi ya Hija na Umra. Ikiwa washirikina watapigana katika miezi hiyo, basi Waumini nao yawapasa wapigane. 6. Kuacha kutoka kwenda pigana na maadui wanauwa pasina nasi kupigana nao ni kuipoteza kheri na wema. Kwa haya inadhihiri kuwa vita vya Islamu vina fadhila katika sababu zinazo pelekea kuanza kwake, na vina uadilifu katika kuviendesha. Viwapi hivi na vita vya mataifa mengine ya zamani na ya sasa! Vita vyao hao ni vya uchafu, na vita vya Islamu ni vya Haki na vyenye fadhila.
Timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ukamilifu, wala yasiwe makusudio yenu ya kidunia kama kutaka umaarufu na kadhaalika. Mkiharimia Hija na Umra akakuzuieni adui njiani basi mtatoka katika Ihram yenu kwa kunyoa nywele. Lakini kabla ya hayo mchinje mnyama aliye mwepesi kumpata, kama mbuzi au ngamia au ng'ombe, na kumtoa sadaka kwa masikini. Wala msinyoe mpaka mtimize haya. Mwenye kuharimia akapata maudhi katika nywele zake kwa maradhi au wadudu hapana ubaya kunyoa. Juu yake hapo atoe fidiya kwa kufunga siku tatu, au kutoa sadaka kuwalisha masikini sita chakula cha kutwa, au kuchinja mbuzi na kumtoa sadaka kwa masikini. Na ikiwa mpo katika amani na salama na hakukutokeleeni adui njiani, na mkakusudia Hija na Umra, na mkajistarehesha kwa kufanya Umra kwanza mpaka ufike wakati wa Hija ndio mharimie, basi inakupaseni kuchinja mbuzi kwa ajili ya masikini na mafakiri wa Makka. Asiye pata mbuzi au hamiliki bei yake afunge siku tatu hapo Makka, na siku saba akisha rejea kwao. Haya ni kwa aliye kuwa hana watu wake Makka. Kwa mwenye watu wake Makka hapana kitu akijistarehesha.