Lakini wao hawaachi kuendelea katika ghasia na inda zao. Kila kikundi katika hao hudai kuwa ni dini yao wao tu ndiyo iliyo sawa. Mayahudi hukuambieni: Kuweni Mayahudi mpate kuhidika na kuongokewa kwenye njia sawa. Na Wakristo nao wanasema: Kuweni Wakristo ndio mpate kuongoka kwenye haki iliyo nyooka. Nyinyi wajibuni kuwa sisi hatufuati hii wala hii kwa sababu dini zote hizo mbili zimekwisha potoka na zimeacha ile asli yake ya kweli, na zimeingia ndani yake ushirikina (upagani), na ziko mbali kabisa na mila ya Ibrahim. Bali sisi tunaufuata Uislamu ndio ulio ifanya mila ya Ibrahim kuwa safi iliyo safika.
Waambieni: Sisi tunamuamini Mwenyezi Mungu, na tunaamini Qur'ani iliyo teremshwa kwetu, na kadhaalika tunaamini waliyo teremshiwa Ibrahim, na Ismail, na Is-hak, na Yaakub na watoto na wajukuu zao, na tunaiamini Taurati ile Mwenyezi Mungu aliyo mteremshia Musa ambayo iliyo kuwa haijakorogwa, na Injili aliyo teremshiwa Isa na Mwenyezi Mungu, ambayo haikukorogwa, na walio pewa Manabii wote kutokana na Mola wao Mlezi. Sisi hatutafautishi hata mmoja kati yao, tukawa tunawakanusha baadhi na kuwaamini wengineo. Na katika haya sisi tunakuwa ndio Waislamu wenye kunyenyekea amri ya Mwenyezi Mungu.
Wao wakiamini imani inayo wafikiana na imani yenu basi kweli wameongoka. Lakini wakikakamia katika inadi yao na kukataa kwao basi hao wamo katika ushindani usio koma, na hawana masikizano nanyi. Mwenyezi Mungu atakutosheni kukulindeni na shari yao, ewe Nabii. Na atakupumzisha na ghasia zao za inadi na upinzani wao. Kwani Yeye ni Mwenye kuyasikia wayasemayo, na Mwenye kuyajua hata yaliomo vifuani mwao.
Waambieni: Hakika Mwenyezi Mungu ametuongoa sisi kwa uwongofu wake mwenyewe, na ametuonyesha hoja zake. Na hapana mbora zaidi kwa uwongofu na hoja kuliko Mwenyezi Mungu. Na sisi hatumnyenyekei ila Mwenyezi Mungu. Na wala hatufuati ila anavyo tuongoa na kutuongoza Yeye. (Hilo ndilo pambo, au batizo, au kutia rangi kwa Mwenyezi Mungu--S'ibghatu Llahi).
Waambieni: Mnajadiliana nasi katika mambo ya Mwenyezi Mungu mkidai kuwa Yeye hakuteuwa Manabii ila kutokana nanyi tu? Na Mwenyezi Mungu ni Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa kila kitu; hawapendelei kaumu fulani akawatupa wengine. Rehema yake humfikia amtakaye, na huwalipa watu wote kwa vitendo vyao, bila ya kuangalia nasaba yao na ukoo wao. Na Yeye ametuongoa kwenye Njia Iliyo Nyooka katika vitendo vyetu. Na ameturuzuku tumsafie niya na vitendo Yeye.
Waambieni: Mnajadiliana nasi katika mas-ala ya Ibrahim, na Ismail, na Is-hak, na Yaakub na watoto na wajukuu zao, mkidai kuwa wao walikuwa Mayahudi au Wakristo kama nyinyi, na ilhali Sisi hatukuiteremsha Taurati na Injili wanazo zitegemea Mayahudi na Wakristo ila baada ya hawa. Na Sisi tulikwisha waelezeni khabari ya hayo. Jee, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Bali hakika Mwenyezi Mungu amekwisha waambieni nyinyi hayo katika vitabu vyenu. Basi msiifiche kweli iliyo andikwa katika hivi vitabu vyenu. Na nani dhaalimu mkubwa zaidi kuliko yule anaye ificha kweli inayo toka katika kitabu chake ambayo naye anaijua. Na Mwenyezi Mungu atakulipeni kwa upotovu mnao ushikilia, kwani Mwenyezi Mungu haghafiliki na mnayo yatenda.
Tena imekuwaje nyinyi Mayahudi na Wakristo kuyajadili mambo ya watu hawa? Kwani watu hawa wamekwisha pita na njia zao. Wao watapata malipo ya a'mali yao waliyo itenda katika uhai wao, wala nyinyi hamtaulizwa juu ya a'mali zao, wala hamtafaidika kwa lolote katika hayo. Nanyi hamtapata malipo ila kwa vitendo mnavyo vifanya nyinyi wenyewe.